Hivi karibuni waziri mkuu, Mizengo Pinda alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema “Wapigwe tu, watakao kataa kutii amri!…” wakati anazungumzia Bungeni vurugu zinazoendelea kutokeza nchini mwetu hivi sasa. Hii ni kauli ya hatari sana kwa usalama wa nchi yetu, na mbaya zaidi kwa mahusiano baina ya raia na jeshi la polisi, ambayo tayari yamesha jeruhiwa kwa muda mrefu. Kwa Mtanzania yeyote aliyekulia Tanzania anajua kwamba jeshi la polisi lina utamaduni wa kupiga raia bila sababu za msingi. Sasa kiongozi mkubwa wa serikali kama waziri mkuu, anapokuja na kauli za kiholela kama hizi, anakuwa hajengi bali anabomoa!
Pinda, akumbuke kwamba nchi inaendeshwa kwa misingi ya sheria na lazima sheria ipewe nafasi ya kufanya kazi yake, na sio ubabe. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 13, Kifungu cha 6B inasema “Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kuteswa kama mtu mwenye kosa, mpaka itakapothibitika anayo hatia kwa kutenda kosa hilo. Pia ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema “Ni marufuku kwa mtu yoyote, kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazoweza kumdhalilisha”.
Najua Pinda alijitetea kule Bungeni kwamba vipengele hivi havihusiani na mtu, amnbaye bado hajakamatwa, sasa kwa maana hiyo Pinda ana halalisha ukamataji wa kutumia nguvu kupita kiasi, ambao Pilisi wetu wamekuwa wanatumia kwa muda mrefu sasa? Binafsi nimesha shuhudia mtu amekamatwa na Polisi katika mazingira ya utulivu na amani kabisa, lakini muda si mrefu nikasikia Polisi wanaanza kusema “hatujalionja hili bado!” na muda si mrefu wakaanza kumpiga virungu vya ugoko mtu yule.
Sasa katika utamaduni kama huu, Pinda anatakiwa awe na busara, ili kusaidia kubadili utamaduni huu, ambao unaenda kinyume na haki za binaadam na hauna nafasi katika Tanzania yetu. Katika bomu lililolipuliwa kwenye mkutano wa CHADEMA kule Arusha, mashahidi mbalimbali wameendelea kujitokeza na kuripotiwa na vyombo mbalimbali kwamba jeshi la Polisi limechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza tafrani baada ya bomu kulipuka.
Nukuu mbalimbali zimeendelea kusema kwamba Polisi walilipua mabomu ya machozi na kuanza kusambaza watu, ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wanahitaji msaada na si mabomu mengine ya ziada. Mpaka sasa bado kuna habari nyingi za kuchanganya kuhusu nini haswa kilitokea Arusha, na ni matumaini yangu kwamba Serikali itafanya uchunguzi wa kutosha, ili kubaini ukweli kwa manufaa ya taifa Zima.
Naomba kumalizia kwa kukumbusha kwamba jukumu moja wapo kubwa katika majukumu ya viongozi wetu, ni kulinda katiba na si kubomoa.
Rungwe Jr.
TheHabari.com