Albino Waanzisha Tuzo za Mashabiki wa Soka Afrika Mashariki

Naibu Katibu wa Chama cha Albino Tanzania, Wilaya ya Temeke, Maria Byabato. (wa pili kutoka kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu tuzo maalum ya soka, wa pili (kulia) ni Mwenyekiti wa chama hicho, Kassimu Kibwe. Kutoka kushoto wa kwanza ni Afisa Mipango wa chama hicho, Cathew Lwali, kulia wa kwanza ni Mweka Hazina wa chama, Said  Ndonge. (Picha na Magreth Kinabo)

Na Lorietha Laurence – MAELEZO
 
CHAMA cha Albino Tanzania, (CCAT) wilaya ya Temeke kimeanzisha tuzo maalum ijulikanyo kwa jina la ‘Tuzo Kwa Klabu za Soka Zenye Mashabiki Wengi Afrika Mashariki’, ili kuhamasisha maendeleo ya soka katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Hayo yalisemwa leo Mwenyekiti wa CCAT Kassim Kibwe wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dares Salaam.

Ambapo alisema uamuzi huo, umeafikiwa baada ya kuona maendeleo ya soka katika nchi za Afrika Mashariki hayaridhishi hasa ukizingatia nchi hizo hazijawahi kushiriki kwenye Fainali za Kombe la Dunia.

Akielezea malengo ya tuzo hiyo alisema ni kuinua klabu za soka zenye mashabiki wengi kwenye eneo hilo ikiwemo klabu ya Yanga na Simba, Tanzania Gor Mahia na AFC Leopards, Kenya na nyingine za kutoka Uganda, Rwanda na Burundi.

Kibwe aliongeza kuwa wamehamasika kuanzisha tuzo hiyo kwa sababu kiwango cha soka katika nchi za ukanda huo hakiridhishi ili kuufanya mchezo huo uhimarike na kuwezesha timu zetu kushirika katika Ligi Kuu  na Kombe la Dunia.

Alisema tuzo hiyo itagharimu pesa za Kitanzania Sh. 6,000,000,000 (bilioni sita) zitakazowekwa kwenye akaunti ya tuzo na mdhamini baadae kukombolewa na mashabiki wa klabu husika kwa kila mmoja kuchangia Tshs 2,000 kupitia mitandao ya simu.

Aidha aliongeza kwa kuwa tuzo hiyo itakombolewa na mashabiki wa Klabu husika kwa kipindi cha miezi mitatu na endapo Klabu itashindwa kuikomboa tuzo hiyo kwa muda uliowekwa watakuwa wameshindwa pia kuiabisha Klabu yao kwa kuikosesha fedha ambayo itafanyiwa mashauri mengine kwa maendeleo ya klabu husika.

Mwenyekiti huyo amewataka wadau wa klabu itakayopata tuzo hiyo kuzingatia harambeee ya kuikomboa kwa kuchangia Sh. 2000 ili kupandisha dhamani ya klabu yao na kuifanya iwe na dhamana kubwa ya kuifanya klabu iweze kukopesha fedha nyingi na kuweza kuvutia wafadhili wakubwa.