Na Magreth Kinabo – Maelezo
JUMLA ya wajasiliamali wapatao 250 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani watapatiwa mafunzo ya elimu ya ujasiriamali, uzalishaji bora wa bidhaa na uundaji wa vikundi vya uzalishaji ili kukidhi oda kulingana na mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo ya muda wa siku tatu kuanzia Juni 25, mwaka huu yatafunguliwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Abdallah Kigoda saa tatu asubuhi katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani jijini Dares Salaam ambapo yatasaidia kukabiliana na changamoto juu ya masuala hayo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa wote (EOTF), Stephen Emmanuel kutipia taarifa yake aliyoitoa leo kwa vyombo vya habari, ambapo alisema mafunzo hayo yanafadhiliwa na mfuko huo unaosimamiwa na Mke wa Rais wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa.
“Elimu inayotolewa inawezesha wanawake wajasiliamli ambao ndio wazalishaji wakuu wa bidhaa za kilimo, ufugaji, sanaa za mikono n.k. kufanya biashara endelevu na kujikomboa kiuchumi, kuondoa ujinga na maradhi katika jamii yetu ya Tanzania – KUPIGA VITA UMASIKINI,” alisema Emmanuel.
Alisema katika mafunzo hayo kutakuwepo na mada za fursa na changamoto za wanawake hao katika biashara, huduma kwa mteja, umuhimu wa viwango vya bidhaa (TBS), Bar Code, stadi za masoko, fursa za mitaji kutoka taasisi za fedha. Mada nyingine ni ubadilishaji ujuzi, haki za wanawake, rasimu ya katiba mpya na kuhamasisha mapambano ya maradhi hatarishi ya saratani ya matiti na uzazi, malaria na ukimwi yanayomaliza nguvu kazi ya taifa.
Aliongeza kuwa mada hizo zitatanguliwa na mchango wa msanii maarufu Judith Wambura “Lady Jay De” kuwahamasisha wanawake kutumia vipaji vyao kujikomboa katika wimbi la umasikini na kujitegemea. Pia atakuwepo mkongwe wa mashairi ajulikanaye kwa jina la Tambalizeni ambaye atatoa ngonjera juu ya uwezeshaji wa wanawake hao kupitia mfuko huo.
Tangu mfuko huo unazishwe mwaka 1997 umeshatoa mafunzo hayo kwa wanawake hao 3,650, ambapo asilimia 85 wanatoka vijijini, pia wanapewa fursa ya kushiriki katika maonesho ya sabasaba na nje ya nchi.
Aidha aliongeza kuwa mpaka sasa EOTF imewezesha wanawake hao zaidi ya 2500 kushiriki kwenye maonesho ya 36 ya sabasaba ya mwaka 2012, ambapo oda walizopata zilifikia thamani ya sh milioni 55.9.