TAARIFA FUPI YA UCHUNGUZI JUU YA MATUKIO YA MIMBA KWA WANAFUNZI WILAYA YA HANDENI, MKOANI TANGA.
UTANGULIZI
Uchunguzi huu umefanyika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga. Uchunguzi umefanyika kuanzia Machi 19, 2013 katika Kata tatu za Wilaya ya Handeni, ambazo ni pamoja na Kata ya Chanika, Kata ya Vibaoni na Kata ya Kidereko.
Uchunguzi huu wa kihabari ni mwendelezo wa utafiti uliofanyika Machi Mwaka jana (2012), kuangalia ukubwa wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia (GBV), katika vipengele vya Ubakaji, Watoto wa Kike Wanafunzi Kulazimishwa Kuolewa, Vitendo vya Ukeketaji, Vipigo kwa Wanawake pamoja na Vitendo vya Utelekezaji Watoto na Wanawake.
Uchunguzi wa pili umefanyika kuangalia mrejesho wa matukio ya mimba na ndoa katika umri mdogo katika maeneo hayo, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kufanyika kwa utafiti wa mwaka jana.
MBINU ZA UCHUNGUZI
Kabla ya kuanza kwa utafiti huu Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kimetoa mwongozo wa nini cha kufuatilia safari hii kwenye eneo husika. Kata ambazo zilitembelewa na mtafiti na vijiji vyake kwenye mabano ni pamoja na Kata ya Kidereko (Komnyang’anyo & Kidereko), Kata ya Vibaoni (Msasa) na Kata ya Chanika (Kwediyamba). Kata hizi ndizo pia nilizitembelea mwaka jana (2012).
Zipo mbinu kadhaa za kihabari ambazo zilitumika ili kupata taarifa hasa kurejea visa mkasa kwa watu ambao wamehusika katika matukio kadhaa ya makosa awali.
MATOKEO YA UCHUNGUZI
Kiujumla matokeo ya uchunguzi yanaonesha kuna mabadiliko tofauti na ilivyokuwa mwaka jana kipindi ambacho ulifanyika uchunguzi wa mwazo (Machi 2012). Matukio ya kesi za mimba yamepungua kutoka shule hadi shule (kwa mujibu wa shule zilizotembelewa) tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Nadhiru Kinyama ni Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, iliyopo Kata ya Kidereko, anasema idadi ya matukio ya mimba shuleni hapo inapungua kwa sasa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, lakini si kwamba matukio hayo yamekoma kabisa.
“Matukio ya mimba kimsingi kwa sasa yanapungua…lakini si kwamba yamekwisha kabisa, tatizo kubwa ni malezi katika familia pamoja na vishawishi vingine,” anasema mwalimu huyo akizungumza shuleni Komnyang’anyo.
Anabainisha kuwa binafsi akubaliani na mtazamo mwingine kwamba umbali wa makazi kwa wanafunzi unachangia mimba…nasema hivyo kwa kuwa kwa mwaka jana mwishoni kuna mfano mzuri, shuleni kwetu yupo mwanafunzi (wa kidato cha pili ‘C’) ambaye anahudumiwa kila kitu na pia yu-karibu na shule lakini amejikuta akipewa mimba na kukatishwa masomo.
Mwanafunzi huyu pia huwezi kumuingiza katika kundi la wanafunzi wenye mazingira magumu ya maisha katika familia zao, nasema hivyo kwa kuwa huyu analipiwa kila kitu, anapewa matumizi yote yanayoitajika na shirika moja linalosaidia wanafunzi wa kike lakini ameshindwa kuendelea baada ya kupewa mimba.
Kesi hii tayari ipo kwenye Serikali ya kijiji kwa hatua zaidi baada ya sisi kutoa taarifa. Sasa watu wanachukulia hatua si kama ilivyokuwa hapo nyuma.Tangu amekuwa huyu Mkuu wa Wilaya mpya (Muhingo Rweyemamu) wananchi wanatoa ushirikiano kwa kesi kama hizi.
Kimsingi ujenzi wa mabweni itakuwa hauweni kwa wanafunzi ambao kwa sasa wanatokea vijiji vya mbali kuja shuleni, vijiji hivyo ni pamoja na Bangu, Kwamagome na Kwakonje.
Mazungumzo ya wanafunzi Hamad Ngomero kidato III, Salome Kalage kidato cha IV, Michael Richard kidato cha I, Mwajuma Munga kidato cha II, Mwajabu Fungo kidato I na Farid Iddy kidato cha IV wote kutoka Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wanasema matukio ya mimba bado yapo shuleni kwao japokuwayamepungua.
Mwajuma Munga anasema matukio hayo bado yapo lakini yamepungua si kama ilivyokuwa hapo nyuma. Naye Salome Kalage anasema mfano kuanzia mwezi Januari 2013 anawajua wanafunzi watatu ambao wamepata mimba na kuachishwa shule. Anawataja wanafunzi hao ni pamoja na Kuruthumu Omar (IV), Elizabeth Hamis (IV) na Docas (III).
Hamad Ngomero anasema tama ya starehe na hali ngumu ya maisha katika familia ndiyo inayowaponza wanafunzi wa kike na hata kujikuta wakitiwa mimba na kukatishwa masomo.
Mwaka 2012 wakati nikipita katika shule hii ilikuwa na jumla ya kesi za matukio ya mimba kwa wanafunzi zilikuwa saba (7). Kwa sasa nilipata wanafunzi watatu tu.
Kwa upande wake; Martin Mwingo ni Mwaliku Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kileleni; ujio wa Mkuu wa Mkoa mpya Handeni umeanza kuonesha mafanikio kwa upande wa matukio ya mimba kwa wanafunzi.
“DC (Mkuu wa Wilaya) wasasa anajitahidi sana kupitia kampeni yake ya “Niache Nisome” anafuatilia kesi za mimba na kuhakikisha wahusika wanapata adhabu kwa mujibu wa sheria…mfano sasa hivi tuna kesi moja tumeletewa hizi ni juhudi za Mkuu wa Wilaya,” anasema Mwingo.
Kesi zinapungua mfano mwaka jana tulikuwa na kesi mbili za mimba lakini mwaka huu (2013) hadi sasa hatujapata kesi ya mimba…lakini pamoja na hayo malezi ya watoto kwa wazazi bado ni tatizo, mtoto ananyenyekea mzazi wake tu dharau kwa watu wengine-haya si malezi. Zamani mtoto anaweza kuadhibiwa na mkubwa yeyote ilimradi awe amekosa, lakini sasa sivyo.
“Mi nashangaa kila uchao watu wanang’ang’ania haki za watoto wasiadhibiwe uweke utaratibu wa kutoa adhabu lakini nashangaa kwanini wasitaje na wajibu wa mtoto hili ni muhimu…tusing’ang’anie haki za mwananafunzi tu tuoneshe na wajibu wake pia,” anasema Mwalimu Mwingo.
Anasema pamoja na juhudi hizo bado utandawazi unaathiri nidhamu za wanafunzi, umiliki wa simu za mkononi matumizi mabaya ya mitandao kama tovuti nayo yanawaharibu wanafunzi, ipo haja ya Serikali kuingilia na kupiga marufuku wanafunzi kumiliki simu shuleni maana simu inamambo mengi sasa.
Fatuma Yusuf (IVB, Sophia Karinga (IVA), Hassan Bakari (IVA), Maimuna Shaban (III), Belisa Omar (I), Hussen Kigoma (III), Catherine Mkanyaje (II), Mariam Mohamed (II) na Asha Hemed (I) katika mazungumzo yao na mtafiti wanasema; Kuna haja ya wanafunzi hasa wa kike kupima ujauzito mara kwa mara.
“Sasa hivi wapo ambao wanapata na kutoa mimba hizo bila uongozi wa shule kujua…sasa hivi tunawajua wanafunzi wawili ambao walipata mimba mwaka huu shuleni kwetu. Mfano Joyce Gasper na Jesca Paul wote wa kidato cha nne wamepata mimba…huenda mwaka huu mimba zikaongezeka zaidi,” anasema anasema Hussein Kigoma.
Eliakimu Kapele ni Makamu wa Shule ya Sekondari Kivesa; anasema linapungu tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma. Mfano mwaka jana tulikuwa na matukio mengi ya kesi za mimba kwa wanafunzi, lakini hadi muda huu kwa 2013 tunayo matukio mawili tu. Na hatu zinachukuliwa maana msukumo unaanzia kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Hii inatokana na Mkuu wa Wilaya wa sasa Muhingo Rweyemamu ametia mkazo sana masuala ya mimba kwa wanafunzi, watu wamekuwa makini na wafuatiliaji.
“Mfano sasa mimba inapotokea kuanzia mzazi wa mtoto aliyetiwa mimba, mtoto mwenyewe na mtuhumiwa wote wanashikiliwa…mi naamini kama adhabu hizi zitaendelea kutolewa ipasavyo watu watanyooka tu,” anasema mwalimu Kapele.
Hata hivyo mwalimu huyo anashauri mabadiliko ya sheria na kanuni za utoro shuleni, anasema maamuzi yamekuwa na mkanganyiko. Mfano kanuni za shule zinaelekeza kuwa mwanafunzi asipo hudhuria shule kwa siku 90 afukuzwe shule. Hili kwa sasa halifanyiki maana limekaa kisiasa zaidi…wanafunzi wanatoroka hatua zinachukuliwa kwa mujibu wa maelekezo lakini baadaye wanarejeshwa kuja kufanya mitihani, hili ni tatizo.
“Inatokea mwanafunzi anabeba mimba na baadaye anarudi shuleni baada ya kujifungua, mwanafunzi kama huyu ni tatizo hawezi kuwa na vurugu sana kinidhamu na wakati mwingine anawavuruga hata wenzake maana anakuwa hana maadili.”
Shule yetu inautaratibu mzuri wa kuhakikisha muda wote unaofaa wanafunzi wanakuwa darasani kupata kilichowaleta hapa shuleni. Lakini huwezi kuamini kuna baadhi ya wanafunzi muda wote wapo huku vichochoroni wanajificha hawaji shuleni, utoro umekithiri! Lakini hawa huenda wakaruhusiwa kuja kufanya mitihani hapo baadaye.
Kanuni za shule mara kadhaa zimewekwa pembeni na siasa kuingizwa kwenye kanuni hizo, hali hii inawapa wanafunzi kiburi na uhuru mkubwa-huwenda wanadhani kufanya hivi ni kuwasaidia lakini ukweli ni kwamba wanawaharibu.
Ofisa Elimu Wilaya ya Handeni, Mgaza Muchiwa anakiri kuwepo na mabadiliko makubwa ya utoro wa mimba ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka jana. “Kimsingi huko nyuma utoro hasa wa mimba ulikithiri kwa wanafunzi wa Sekondari na Msingi, lakini hali ya sasa ni tofauti. Kuna mabadiliko kampeni ya ‘Niache Nisome’ imesaidia sana…kwa sasa wengi wanaohusika na kuwatia mimba wanafunzi wanapelekwa mahakamani,” anasema Muchiwa.
Anasema zoezi la kamatakamata lililokwenda sambamba na kampeni ya ‘Niache Nisome’ na watu hufikishwa kwenye hatua mbalimbali limesaidia hivyo mambo yanabadilika. Kwa mantiki hiyo waweza kuona kuanzia Januari 2013 hadi sasa (Machi) sijapokea kesi hata moja ya mimba.
Tunachokifanya sasa ni kutoa elimu zaidi kwenye mikutanyiko ya jamii kupitia viongozi wa ngazi mbalimbali za halmashauri, ili kuhakikisha tunafanikiwa zaidi tumeanza mkakati wa kuwajengea uwezo wananchi na shule. Hii ni kukabiliana na baa la njaa ambalo limekuwa likijitokeza mara kadhaa.
“Unajua mtu anapokuwa na njaa kushawishika ni rahisi…na Handeni kuna njaa sasa hali kama hii yaweza kuathiri pia sekta ya elimu, tumejipanga kuimarisha kilimo cha mazao kama mahindi na mtama shuleni ili wanafunzi wawe na uhakika wa chakula wawapo shuleni,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Wilaya ya Handeni.
Ofisa Elimu Taaluma, Basil Mrutu anasema kwa mwaka jana kwa mujibu wa takwimu zao walikuwa na ripoti za mimba 26 kwa Wilaya nzima, lakini tangu Oktoba 2012 hadi sasa hawajapata kesi za matukio ya mimba.
Simon Mdaki ni Mkuu wa Idara ya Sekondari Wilaya ya Handeni; anasema kuwa “Halmashauri imeandaa matrekta 7 ambayo shule zitapewa kipaumbele cha kuyatumia ili kuweza kuendesha kilimo kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.
Wakati mwingine wananchi wamekuwa wakiibua mradi wa ujenzi kupitia asasi anuai na halmashauri kuunga mkono ujenzi huo wa mabweni. Anasema Shule ambazo zimenufaika na mradi huo wa mabweni ni pamoja na Sekondari ya Kwamsisi iliyosaidiwa na TANAPA, Sekondari ya Kisaza kwa msaada wa World Vision, Sekondari ya Misima kwa msaada wa Kanisa (Pentecostal), pamoja na Sekondari ya Chogo iliyosaidiwa kujengewa bweni na UNHCR.
lakini pamoja na hili umbali kutoka makazi ya wanafunzi na shule ni tatizo lingine-na hili tayari tunalifanyia kazi hadi sasa kuna shule kadhaa ambazo zimefanikiwa kujengewa mabweni ama kwa ushirikiano kati ya wananchi na halmashauri au wafadhili,”.
Kwa upande wa Polisi Wilaya ya Handeni nao takwimu zinaonesha kupungua kwa matukio ya kesi za kubakwa wanafunzi na mimba ukilinganisha na ilivyokuwa kwa mwaka jana.
Zuber Chembera ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni (OCD), anakiri kupungua kwa matukio ya kesi za mimba/kubakwa kwa wanafunzi kulingana na takwimu zao. Anasema kwa mwaka 2012 hadi mwezi Novemba walikuwa na jumla ya matukio ya kesi kama hizo 66. Lakini anasema kwa mwaka huu (Machi, 2013) kuna jumla ya matukio ya kesi hizo 14 tu.
Anasema elimu inayotolewa na Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Handeni imesaidia. “Kesi zinazotufikia hapa huku zikiwa na ushaidi wa kutosha tunazipeleka mahakamani, zile zinazokuwa hazina ushaidi wa kutosha tunajaribu kuzifuatilia kiuchunguzi kwa mujibu wa taratibu zetu. Lengo letu kupitia Dawati la Jinsia na Watoto ni kuhakikisha tunapunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo hivyo.
Anasema maranyingi ushahidi wa kesi kama hizo pia umekuwa ukiharibiwa na wahusika kabla ya kufika mahakamani, wanaweza baada ya kesi kufunguliwa wakashawishiana na kukaa nje bila ya sisi kujua na hivyo kupotea wote.
Muhingo Rweyemamu ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni kwa sasa na mwanzilishi wa kampeni ya ‘Niache Nisome’ kupambana na matukio ya kesi za mimba kwa wanafunzi ambazo aliingia katika wilaya hiyo zikiwa zimeshamiri.
Akizungumzia kampeni ya ‘Niache Nisome’ aliyoianzisha muda mfupi baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuiongoza wilaya hiyo, anasema kampeni yake imekuwa na mafanikio kwani licha ya matukio ya mimba kupungua wananchi wameipokea vizuri kampeni hiyo.
Anaongeza kuwa wananchi hasa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiripoti matukio ya mimba na kutoa ushirikiano pale inapoitajika ili wavunjaji sheria kwa wanafunzi waweze kuadhibiwa kitendo ambacho hapo awali kilikuwa kigumu, na hata wengine kushirikia mikakati ya kuwaachisha masomo wanafunzi.
“Nina furahi kuwa muitikio wa kampeni ya ‘Niache Nisome’ katika maeneo mengi ya wilaya yangu imepokelewa vizuri, wananchi wanaanza kutambua umuhimu wa elimu na wanatoa ushirikiano kwa wale wachache wanaokwenda kinyume kwa kuwakatisha masomo wanafunzi hasa wa kike…jamii ya hapa wengi wao mwanzoni ilikuwa ni kitu cha kawaida mwanafunzi kulala nje pasipo idhini ya wazazi wake,” anasema Rweyemamu akizungumza.
Akizungumzia utekelezaji wa kampeni hiyo Mkuu wa wilaya alisema licha ya kamatakamata iliyokuwa ikifanyika kwa wazazi, wanafunzi na watu waliyokuwa wakisababisha mimba kwa wanafunzi viongozi na watendaji anuai wa halmashauri hiyo walizunguka maeneo mengi na kutoa elimu juu ya umuhimu wa elimu kwa jamii zima.
“Tulikamatana sana mwaka jana kuanzia mwezi wa nane na kwa muda mfupi tulikuwa tuna watuhumiwa 80 wakiwemo wazazi, watu waliokuwa wakidaiwa kusababisha mimba kwa wanafunzi pamoja na wanafunzi wenyewe…mimi mwenyewe nilitembelea baadhi ya shule nikitoa elimu lakini baadaye walielewa licha ya uwepo wa changamoto kadhaa,” anasema kiongozi huyo wa Wilaya ya Handeni.
Aidha akifafanua zaidi alisema ipo haja ya kampeni hiyo kugeuzwa taasisi na kuanza kufanya shughuli zake nchi nzima ili kampeni kama hiyo iweze kuyanufaisha maeneo mengi ambayo yamekuwa na mwamko duni wa elimu kwa jamii. Aliongeza kuwa faida ya kampeni hiyo haipiganii elimu kwa mtoto wa kike pekee kwani inagusa maeneo mengine pia kama miundombinu ya shule, vitendea kazi na vifaa vingine muhimu kwa shule kiujumla.
Kwa upande wa Mahakamani, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi wa Wilaya, Patrick Maligana anasema licha ya takwimu zao kuonesha kesi za mimba/kubaka wanafunzi kupungua bado suala la kuharibika kwa ushaidi wa kesi za mimba ni changamoto kwao. Anasema kesi nyingi ya kubaka/mimba wanafunzi zimekuwa zikishindwa kufanikiwa hadi kwenye hukumu kutokana na utaratibu wa kuvuruga ushahidi.
“Kesi nyingi ambazo zinatufikia zinashindwa kufikia hukumu maana mashahidi wanashindwa kuthibitisha pasipo shaka…nyingi zinaharibika sababu hawataki kusema ukweli, hivi karibuni nililazimika kuwaweka ndani wawili (mashahidi) kwa kuwa wanadanganya. Unakuta maelezo aliyotoa polisi ni mengine na akifika huku anageuka,” anasema Hakimu Maligana.
Anasema awali kikwazo kilikuwa kwa upande wa wazazi na walimu, lakini walimu na wazazi wameacha usumbufu huo hivyo imebaki kwa wanafunzi pamoja na watuhumiwa wapenzi wao. Anaongeza kuwa licha ya matukio hayo kupungua changamoto bado zipo.
Takwimu za kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2012 mahakama ilipokea kesi 10 za tuhuma za mimba/kubaka kwa wanafunzi, huku kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2013 ni jumla ya kesi 6 tu zimepokelewa katika mahakama hiyo huku, sita za mwisho zikiwa katika hatua tofauti.
1.0 WATU WALIOHOJIWA KATIKA UCHUNGUZI HUU
1. Muhingo Rweyemamu, Mkuu wa Wilaya ya Handeni (0754303552)
2. Basil Mrutu, Ofisa Elimu Taaluma (0715387557)
3. Zuber Chembera, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni, (0786807593)
4. Patrick Maligana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi Wilaya, (0787332332)
5. Mgaza Muchiwa, Ofisa Elimu Wilaya ya Handeni (0717478740)
6. Eliakimu Kapele, Makamu wa Shule ya Sekondari Kivesa (0754217741)
7. Martin Mwingo, Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kileleni (0713711373)
8. Nadhiru Kinyama, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo (0713057905)
9. Fravianu Magesa, Dawati la Jinsia na Watoto, Kituo cha Polisi Handeni (0759057505)
10. John Tisky Katibu Tawala Wilaya Handeni (0784812597)
11. Simon Mdaki, Ofisa Elimu Sekondari Handeni (0784387557)
12. Yusuf S. Nkumulwa – Mwenyekiti Serikali ya Kijiji cha Kwediyamba (0656411200)
13. Ramadhan majogo – Mratibu Elimu Kata Chanika (0784701441)
14. Mwajab Zuberi – Mwananchi 0754234410
15. Mwinjuma Magalu –Mwanafunzi aliyetelekezwa
16. Amina Mohamed –Mwanakijiji Msasa
17. Fatuma Mohamed – Mwanakijiji Komnyang’anyo
18. Fatuma Yusuf – Mwanafunzi (IV B)
19. Sophia Karinga- Mwanafunzi (IVA)
20. Hassan Bakari – Mwanafunzi (IVA)
21. Mariam Mohamed – Mwanafunzi (II)
22. Swaumu Bakari – Mwanafunzi (III)
23. Hussen Kigoma – Mwanafunzi (III)
24. Belisa Omar (I) Mwanafunzi
25. Habiba Mohamed – Mwanafunzi (IV)
26. Maimuna Shaban – Mwanafunzi (III)
27. Asha Hemed –Mwanafunzi (I)
28. Hamad Ngomero –Mwanafunzi kidato III
29. Salome Kalage –Mwanafunzi kidato cha IV
30. Michael Richard Mwananchi
31. Mwajuma Munga –Mwanafunzi kidato cha II
32. Mwajabu Fungo –Mwanafunzi kidato I
33. Farid Iddy –Mwananchi Handeni
NB
Si wahojiwa wote wameingizwa kwenye orodha hii, kwani wapo wananchi ambao wametoa taarifa lakini walikataa kutajwa majina yao na taarifa zao kuingizwa kwenye uchunguzi kadri ya umuhimu wake.
Imeandaliwa na JOACHIM MUSHI, kutoka wavuti ya habari,
THEHABARI.COM (www.thehabari.com), Box 18180, Dar es Slaam.
Mawasiliano: mushi@dev.kisakuzi.com , 0717 030 066 / 0756 469 470.