MECHI ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kundi C, Kanda ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa jana (Juni 16 mwaka huu) imeingiza sh. 502,131,000 kutokana na watazamaji 57,203. Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 76,596,254.24 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 7,809,104. Asilimia 15 ya uwanja sh. 62,658,846.26, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 83,545,128.35 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 20,886,282.09.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 250,635,385.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 12,531,769.25 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF. Mechi iliyopita ya Stars dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) kwenye uwanja huo iliingiza sh. 226,546,000.
PONGEZI KWA WASHABIKI KUIUNGA MKONO STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa juzi (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwitikio wa washabiki katika mechi hiyo ilikuwa ni moja ya chachu ya kiwango kilichoonyeshwa na Taifa Stars, kwani walishangilia mwanzo hadi mwisho licha ya kupoteza kwa mabao 4-2.
Ni matarajio utakuwepo mwitikio kama huo huo katika mechi ijayo ya Taifa Stars ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Nyumbani (CHAN) dhidi ya Uganda (The Cranes) itakayochezwa Dar es Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu. Stars itaingia tena kambini Julai 4 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo.