Timu ya EAC ya Waangalizi wa Uchaguzi Kenya Yaandaa Ripoti

Dk Julius Rotich

Na Mtuwa Salira, Arusha

TIMU ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya Waangalizi wa Uchaguzi wa Kenya uliomalizika hivi karibuni inakutana mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kufanya tathmini ya uchaguzi huo mkuu kisha kuanda ripoti kwa ajili ya Baraza la Mawaziri wa EAC kabla ya kukabidhiwa kwa wakuu wa nchi.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili mafanikio, changamoto na uzoefu uliopatikana kutokana na uchaguzi huo kwa ajili ya kufanya vizuri kwa chaguzi zijazo katika kanda hiyo, kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Dk Julius Rotich.

Warsha hiyo ya siku mbili pia inahudhuriwa na wawakilishi kutoka tume za uchagzi za EAC, Tume za Taifa za Haki za Binadamu, Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na mwaziri wanaohusika na wizara za Afrika Mahariki, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).

“Ripoti hii ina umuhimu mkubwa kuhakikisha kwamba tunafanya maendeleo katika misheni zetu za timu za ungalizi wa uchaguzi kwa ajili ya mafaa ya kanda yetu,” Dk. Rotich alisema katika ufunguzi wa warsha hiyo ambayo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Timu ya Uangalizi ya EAC, Abdulrahman Kinana.

Dk. Rotich pia alisisitiza nchi wanachama wa EAC kutoa kipaumbele kwa timu za uangalizi wa uchaguzi kwa kuzipatia fedha za kutosha.

“Kwa uzoefu uliopatikana Kenya juu ya ufadhili unaonyesha kwamba wakati umefika kwa nchi wanachama kufikiria timu za uangalizi wa uchaguzi ili kupewa kipaumbele kwa kuzipatia fedha za kutosha,” aliwaambia wajumbe.

Alisema kwamba hatua hiyo pia itapunguza utegemezi wa wafadhili juu ya shughuli hiyo muhimu inayohusu pia mtangamano katika kanda hiyo. Kwa mujibu wa maafisa wa EAC, hivi sasa bajeti kwa ajili ya timu za uangalizi wa uchaguzi inategemea zaidi wafadhili kwa shughuli na mipango yake.

Timu za uangalizi wa uchaguzi wa Kenya zipatazo 50 ziliwasili nchini humo kwa kazi hiyo wiki mbili kabla ya uchaguzi wenyewe.