Kauli ya Rais Kikwete Juu ya Mlipuko wa Bomu Mkutano wa Chadema

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa taarifa za shambulio la mlipuko lililotokea katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mjini Arusha jioni ya Juni 15, 2013, tukio ambalo limesababisha vifo vya watu wawili na majeruhi ya Watanzania kadhaa.

Aidha, Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa wote na pia ametuma pole nyingi kwa majeruhi ambao wameumizwa na kujeruhiwa katika tukio hilo ovu na katili.
Vile vile, Rais Kikwete amewatumia salamu za pole viongozi wa CHADEMA kufuatia tukio hilo la woga mkubwa na pia kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki za kuchunguza kwa haraka, kubaini, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na tukio hilo, wawe watu wa ndani ya nchi ama nje ya nchi.
Katika salamu zake za rambirambi na za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Magesa Mulongo, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa shambulio la mlipuko lililotokea katika mkutano wa CHADEMA mjini Arusha jioni ya leo, tukio ambalo limesababisha vifo na majeruhi ya Watanzania wenzetu.”
Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Magesa Mulongo salamu zangu za rambirambi kufuatia vifo na pole nyingi kutokana na majeruhi katika tukio hilo na naomba kupitia kwako unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa na pole nyingi sana kwa majeruhi.”
“Kadhalika naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kutokana na tukio hilo. Naomba uwajulishe kuwa uchungu wao ni uchungu wetu sote na msiba wao ni msiba wetu pia. Nataka wajue kuwa tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi na huzuni mkubwa,”amesema Mheshimiwa Rais Kikwete.
Rais Kikwete amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Arusha: “Kadhalika, nimeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka kuwasaka wahusika, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Aidha, nawataka viongozi wa Serikali ngazi ya kitaifa, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arusha mjini kuhakikisha kuwa majeruhi wote wanapata matibabu ya haraka na huduma za tibabu stahiki.”
Aidha, Rais Kikwete ametoa wito maalum kwa wananchi akisema: “Kwa wananchi wenzangu, Watanzania wenzangu, napenda kutoa wito wa kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi yao vizuri ili tuweze kuwabaini waovu waliofanya kitendo hiki.”
“Natambua kuwa yatakuwepo maneno mengi na hisia mbali mbali zitakazojaribu kulielezea tukio hili ovu na katili kwa njia mbali mbali. Nawasihi tujiepushe na kuchukua dhana na hisia zetu au maneno ya watu wengine kuwa ni ukweli wa tukio hili. Tujipe nafasi ya kutafakari vizuri na kufanya uamuzi ulio bora.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Mimi siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”
“Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, naomba tuzinduke, ili tusiwape nafasi watu hawa waovu ya kuweza kutimiza malengo yao ya kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu kwa kuleta mifarakano baina yetu. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.”