WATU wengi walikosoa upandishaji wa kodi na ushuru wa bidhaa na huduma kwamba utawadidimiza walalahoi. Bajeti ya 2013/14 iliyotangazwa bungeni juzi na Serikali, imesababisha malalamiko na manung’uniko kutoka kila upande wa nchi, huku baadhi ya wasomi, wanasiasa na wananchi wakiiponda kwamba haiwezi kubadili hali ya maisha ya watu wa chini.
Wengi wanakosoa nyongeza ya kodi na ushuru mbalimbali ambazo wanasema zinazidi kudhoofisha hali ya watu wa chini, kwani gharama za maisha zitazidi kupanda na kwamba hali hiyo inawaneemesha walionacho.
Katika maoni yao kuhusu bajeti hiyo iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, wapo waliokosoa vikali misamaha ya kodi ambayo wameitaja kwamba inadhoofisha uchumi wa nchi.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi aliuambia mkutano wa wadau wa uchumi ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu (KPMG) jana jijini Dar es Salaam kwamba, Serikali imeshindwa kukusanya kodi kwa wawekezaji wakubwa.
“Misamaha ya kodi inatolewa kwa wawekezaji wakubwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inasababisha mzigo kwa Serikali. Hizi kampuni kama za simu na madini zinapokuja kuwekeza zinatafuta faida, hakuna sababu ya kuzisamehe kodi,” alisema Profesa Moshi.
Mchumi huyo alikosoa upandishaji wa kodi kwenye mafuta akisema kuwa itapandisha mfumuko wa bei kwa wananchi wa chini. “Huwezi kupandisha kodi ya mafuta, kwani ni chanzo cha kukua kwa mfumuko wa bei kwa kaya. Nilishafanya utafiti katika hilo… ni kweli mfumuko umeshuka, lakini kwa ngazi ya kaya bado bei ya bidhaa haijashuka. Tuna bahati tu mvua imenyesha mwaka huu,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe alisema ni bajeti nzuri ambayo inalenga kuchochea maendeleo. Alisema ili kuhakikisha mapato mengi yanakusanywa ni lazima kuendana na ukuaji wa teknolojia yenye lengo la kuwabaini wanaokwepa kodi. “Wale ambao hawataki kulipa kodi kwa kutumia mifumo mipya, TRA itawabaini na kuongeza mapato ya taifa,” alisema Profesa Wangwe.
Wasomi wengine
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi alisema Serikali imeendeleza utaratibu aliouita kuwa ni mbovu wa kutegemea kukusanya kodi kutoka vyanzo vya anasa.
“Unapoweka kodi katika sigara, vinywaji na kutuma fedha kwa njia ya simu bado si sahihi, kwani vitu hivi vinawahusu watu wa hali ya chini hivyo unaendelea kuwaumiza wananchi wenye hali ngumu ya maisha,” alisema Dk Ngowi.
Naye Mwenyekiti wa Infotech Investment Group, Ali Mufuruki alisema suala la matumizi linatakiwa kuangaliwa upya kwa sababu hakuna tofauti ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Sikuona kama wizara zitaleta manufaa tunayoyategemea kwa sababu rushwa bado ni tatizo katika utekelezaji wa sheria ya ununuzi wa umma,”alisema Mufuruki na kuongeza: “Kunatakiwa kuwepo kwa uwazi katika matumizi ya fedha za wakala mbalimbali za Serikali na bajeti zake ziwe zinapitiwa na Bunge tofauti na inavyofanyika sasa ambapo hupitiwa na bodi zao”.
Mkurugenzi wa Kodi wa Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya Ernst & Young, Laurian Justinian, alisema ipo haja kwa Serikali kuweka utaratibu utakaomwezesha kila mwananchi kuchangia kodi kulingana na kipato chake.
Alisema suala la kuondoa kodi kwenye bajaji na bodaboda siyo sahihi kwani wanaoendesha biashara hizo wana vipato vikubwa ikilinganishwa na mtu aliyeajiriwa kwa kipato cha Sh150,000 kwa mwezi. Mkurugenzi wa Kodi wa KPMG, David Gachewa alisema hatua ya Serikali kupunguza kodi kwa kampuni za ndani ili zishindane na zile za nje haitakuwa na tija kwani itaathiriwa na misamaha ya kodi.
“Waziri wa Fedha ameshusha ushuru wa kampuni za ndani ili zishindane na za nje, lakini bado misamaha mikubwa ya kodi inaongeza utegemezi kwa wahisani. Hata wigo wetu wa ukusanyaji wa kodi bado ni mdogo,” alisema Gachewa. Alisema kitendo cha kuongeza kodi ya mafuta kitasababisha kupanda kwa mfumuko wa bei, hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa Mtanzania wa kipato cha chini.
Rasilimali za nchi
Wataalamu hao wa masuala ya uchumi walishangazwa na bajeti ya Serikali kushindwa kuweka bayana jinsi sekta muhimu na rasilimali mpya za nchi zitakavyotumika kukuza uchumi wan chi.
Profesa Moshi yeye alisema anashangazwa na Serikali kutotaja mikakati ya Taifa kufaidika na gesi iliyopatikana Mikoa ya Kusini. “Nimeshangaa kutosikia Waziri wa Fedha akigusia mkakati wa kutumia gesi… Uganda wenzetu wameweka mikakati ya kutumia rasilimali mpya ya mafuta, lakini sikuona kwetu Waziri akizungumzia,” alisema Profesa Moshi.
Akitaja changamoto za uchumi wa Tanzani, Profesa Moshi alitahadharisha kuwa gesi hiyo itakuwa laana kama mikataba ya uchimbaji itafanywa kuwa siri.
Kwa upande wake Ali Mufuruki alisema sekta za miundombinu, elimu na kilimo zinatakiwa kuangaliwa upya kwa sababu hakuna mkakati maalum unaoonyesha kuzisaidia sekta hizo. Kwa mujibu wa Mufuruki, suala la kupunguza kodi kwenye vifaa vya reli halitoshi badala yake kunatakiwa uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo kwani itasaidia kupunguza garama za usafirishaji kwa asilimia 70.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz