Daraja la Kigamboni kuanza kujengwa Desemba


Mmoja wa wafanyakazi wa NSSF ndani ya Banda lao katika viwanja vya Saba Saba, akieleza namna ya muonekano wa Daraja la Kigamboni litakavyokuwa na namna litakavyofanya kazi baada ya kukamilika.

Na Joachim Mushi

UJENZI wa Daraja ambalo limekuwa likisubiriwa kwa hamu na wananchi wengi hasa wakazi wa Mji wa Kigamboni unatarajia kuanza Desemba mwaka huu. Akizungumza na mtandao wa dev.kisakuzi.com jana kwenye viwanja vya Saba Saba ndani ya Banda la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Felix Uiso alisema taratibu za awali zimekamilika ikiwa ni pamoja na kuandaa michoro ya daraja lenyewe.

Aidha alisema ujenzi huo utachukua muda wa miaka mitatu kabla ya kukamilika huku ukitarajiwa kugharimu fedha kiasi cha dola za kimarekani milioni 130. Akifafanua zaidi alisema daraja hilo la kisasa litakuwa na barabara tatu za kwenda na kurudi pamoja na njia maalumu ya waenda kwa miguu.

Hata hivyo alisema mara baada ya kukamilika daraja hilo NSSF itaanza kutoza malipo kwa kila chombo cha moto kitakachokuwa kikipita katika daraja hilo ili kurejesha gharama zao na baada ya hatua hiyo kukamilika kwa makubaliano, daraja litakabidhiwa serikalini ili liweze kuendeshwa kwa utaratibu utakaokuwa ukifaa.