Rais Kikwete Aalikwa Kuhudhuria Mkutano wa G8

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amealikwa kuiwakilisha Tanzania na Afrika katika shughuli za Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Nchi Zenye Viwanda Vingi Duniani – G8 wa mwaka huu unaofanyika London, Uingereza.
Rais Kikwete pamoja na ujumbe wake, aliondoka nchini usiku wa kuamkia leo, Ijumaa, Juni 14, 2-13 tayari kwa mkutano uliopangwa kufanyika kesho, Jumamosi.
Rais Kikwete ambaye pia alihudhuria mkutano wa mwaka jana wa G-8 Marekani kwa mwaliko wa Rais Barack Obama, amealikwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa David Cameron kuhudhuria mkutano wa mwaka huu.
Rais Kikwete ambaye atashiriki katika kikao cha kujadili ukuaji wa uchumi ataungana na Rais John Mahama wa Ghana, Rais Alpha Conte wa Guinea, Rais Hassan Sheikh Mahmound wa Somalia na Rais Blaise Compaor’e wa Burkina Faso kushiriki katika kikao hicho.
Rais Kikwete ameandamana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.