RCL Yaingia Hatua ya Tatu Wikiendi Hii

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

MECHI za kwanza za hatua ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao zinachezwa wikiendi hii kwenye viwanja vinne tofauti.

Mechi za kesho (Jumamosi) ni kati ya Kariakoo ya Lindi na Friends Rangers ya Dar es Salaam utakaochezwa katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi wakati Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Kimondo SC na Njombe Mji.

Timu za Machava FC ya Kilimanjaro na Stand United FC ya Shinyanga, Polisi Jamii ya Mara na Katavi Warriors ya Katavi zilizokuwa zipambane kesho mechi zao zimesogezwa mbele hadi keshokutwa (Jumapili). Mechi hizo zimesogezwa kutokana na viwanja vya Ushirika mjini Moshi na Karume mjini Musoma kuwa na shughuli nyingine za kijamii.

Hata hivyo, TFF imesisitiza kuwa ikibainika kuwa viwanja hivyo havikutumika kwa shughuli za kijamii siku hiyo ya Jumamosi, hatua kali zitachukuliwa kwa wanachama wake (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika).

Mechi za marudiano za hatua hiyo ya tatu zitachezwa Juni 19 mwaka huu. Hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.

RAMBIRAMBI MSIBA WA ABDALLAH MSAMBA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Pan Africans, Simba na Taifa Stars, Abdallah Msamba kilichotokea juzi usiku (Juni 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Msamba akiwa mchezaji, na baadaye kocha wa timu kadhaa alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Villa Squad, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Msamba, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na klabu ya Villa Squad na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko ya mchezaji huyo yamefanyika leo (Juni 14 mwaka huu) katika makaburi ya Ndugumbi mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo wachezaji wa zamani na viongozi mpira wa miguu nchini. Mungu aiweke roho ya marehemu Msamba mahali pema peponi. Amina