MACHO na masikio ya Watanzania leo yataelekezwa kwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakati atakapoisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kuanzia saa 10.00 jioni bungeni, mjini Dodoma.
Sambamba na Mgimwa, pia mawaziri wa fedha za nchi za Kenya na Uganda nao katika muda huo watasoma bajeti za nchi zao.
Waziri mpya wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich atasoma bajeti ya kwanza ya nchi hiyo ikiwa chini ya utawala mpya wa Rais Uhuru Kenyatta wakati ya Uganda itasomwa na Waziri wa Fedha, Maria Kiwanuka.
Mwelekeo wa Bajeti
Dk Mgimwa aliwaambia waandishi wa habari, Dodoma jana kuwa Serikali imetenga kiasi cha Sh18.2 trilioni kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha wa 2013/14.
Alisema wameweka vipaumbele kadhaa ambavyo ni nishati vijijini, miundombinu, maji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Bajeti hiyo itatanguliwa na ile ya mwelekeo wa hali ya uchumi ambayo itasomwa asubuhi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Dk Mgimwa alisema wananchi hasa wa vijijini watapata huduma ya maji hasa baada ya kuongezwa Bajeti ya Wizara ya Maji.
Awali, wabunge waligomea Bajeti ya Maji ya Sh398 bilioni kabla ya kuongezwa hadi kufikia Sh582.5 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh184 bilioni.
Waziri Mgimwa alisema pia kuwa suala la nishati ya umeme ni kipaumbele kingine cha Serikali na kwamba itaisambaza katika maeneo mbalimbali nchini na zaidi katika maeneo ya vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Alisema kipaumbele kingine ni usambazaji wa pembejeo za kilimo vijijini ili kuwasaidia wakulima kulima mazao bora. Pia alisema katika mwaka huu wa fedha Benki ya Wakulima itaanzishwa ili kutoa mikopo yenye unafuu ya kilimo.
Aidha, Serikali ilikwishatangaza vipaumbele vingine ambavyo ni ujenzi wa Bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Bagamoyo, reli, elimu, Mfumo wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT), afya na ujasiriamali.
Katika bajeti iliyopita, vipaumbele vya Serikali vilikuwa kuimarisha miundombinu ya uchumi ikijumuisha umeme, barabara, reli, bandari na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha.
Mwelekeo wa uchumi
Dk Mgimwa alisema uchumi wa nchi umekua kwa asilimia 6.9, wastani ambao ni mzuri na kuongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la karibu Sh1.84 bilioni katika bajeti na kufikia Sh18.2 trilioni.
Udhibiti wa fedha za Serikali
Kuhusu kudhibiti ufujaji wa fedha, Dk Mgimwa alisema: “Tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba watu wasiokuwa na uaminifu wanachukuliwa hatua kali tena kwa haraka.”
Alikiri kuwapo kwa upungufu katika kufikisha fedha za miradi kwa wakati na kwamba hilo linasababishwa na ufinyu wa bajeti na makusanyo.
Moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti Kitengo cha Ununuzi hasa wa magari ya Serikali na katika hotuba yake bungeni alisema: “Ununuzi wa magari ni eneo linalotumia fedha nyingi za umma na kutokana na hilo, Serikali imeona kuna umuhimu wa kuweka utaratibu bora utakaowezesha kupata thamani ya fedha katika ununuzi wa pamoja na matumizi ya magari yake.
Deni la Taifa
Kuhusu deni la taifa, Dk Mgimwa alisema halina shida kwani tofauti na nchi nyingine, nchi bado inakopesheka. Kwa mujibu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni, deni hilo limefikia Sh21.028 trilioni bila dhamana ya Serikali kwa mashirika ya umma na binafsi hadi kufikia Desemba 2012, kati ya fedha hizo, asilimia 75.97 ni deni la nje.
Waziri Mgimwa alisema Serikali imeanza kulipa na kuanzia Julai 2012 hadi Aprili 2013, malipo ya madeni yamefikia Sh1,666.77 bilioni na kati ya hizo, deni la nje lililolipwa ni Sh213.57 bilioni, na Sh1,453.20 bilioni ni deni la ndani.
CHAZO/Kusoma zaidi: www.mwananchi.co.tz