Sherehe za Kuwashukuru Wachangia Damu Juni 14

TANZANIA kupitia Mpango wa Damu Salama Tanzania itaungana na nchi nyengine Duniani katika sherehe za Kuwashukuru na kuwatambua Wachangia Damu Duniani siku ya Ijumaa ya tarehe 14 Juni, 2013 ambapo kitaifa sherehe hizo zitafanyika katika viwanja vya Mkendo Wialyani Musoma, mkoani Mara huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri mwenye dhamana Katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Mh. Dk. Hussein Mwinyi.

Kwa Mujibu wa Mpango wa Damu Salama Tanzania, wananchi ambao wako katika mikoa mengine nje ya kanda ya ziwa wanaweza kujumuika na vituo vya Damu Salama vilivyo katika kanda zao ili kuweza kusheherekea na kujitolea damu siku hiyo.

Aidha, sehemu zilizoanishwa na Mpango wa Damu Salama Tanzania ambapo sherehe hizo zitafanyika Kimkoa ni Makao Makuu ya Mpango wa Damu Salama Tanzania, Ilala Mchikichini kwa Mkoa wa Dar es salaam, Viwanja vya Tangamano kwa Mkoa wa Tanga, Mkoani Tabora Katika Kituo cha Damu Salama Kitete, Viwanja vya Luanda Nzovwe Jijini Mbeya, Kwa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi sherehe zitafanyika katika Bustani ya Mkapa, Morogoro katika Kituo cha Damu Salama Rwegosore, na Mkoani Lindi katika kituo cha Damu Salama Ilulu.

Sherehe hizo za Kila mwaka zinalengo la kuamsha ari pamoja na kuongeza uwelewa juu ya mahitaji ya damu na umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya watu wanaohitaji damu duniani ikiwa pamoja na kuwashukuru na kuwapongeza wachangia damu wote duniani.

Kidunia sherehe hizi zitafanyika Jijini Paris, Ufaransa chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ikishirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC), Shirikisho la Kimataifa laTaasisi za Kuchangia Damu (IFBDO), na Jumuiya ya Kimataifa Mpango wa Damu Salama (ISBT). Ujumbe wa Mwaka huu ni TOA ZAWADI YA MAISHA. CHANGIA DAMU.

Rafiki wa Damu Salama Tanzania inawaomba watanzania wote kujitokeza kwa wingi siku ya Ijumaa kuweza kujumuika pamoja katika sherehe hizi muhimu ambazo zinagusa moja kwa moja maisha ya mwanadamu. Mahitaji ya damu nchini bado ni makubwa na wahitaji wamekuwa wakiongezeka kila siku kutokana na Uzazi kwa kina mama, ajali na magonjwa ya saratani. Kama asilimia 1% tu ya watanzania watajitolea kutoa damu kwa mwaka basi Tanzania itaweza kuondokana na tatizo hili la upungufu wa damu.