Hatimaye Wilfred Rwakatare Aachiwa kwa Dhamana, Mwenzake Aendelea Kusota

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Rwakatare

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam, imemwachilia kwa dhamana Mkurugenzi wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Rwakatare mara baada ya kutimiza masharti ya dhamana iliyofunguliwa leo.

Miongoni mwa masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama na Rwakatare kuyatimiza yote na wadhamini wake ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili ambao wamesaini bondi ya sh milioni 10 na yeye mwenyewe kujidhamini.

Masharti mengine ya dhamana hiyo ambayo ametimiza ni pamoja na Rwakatare kukabidhi mahakamani hati ya kusafiria na kutosafiri nje ya Dar es Salaam bila taarifa. Hata hivyo mshtakiwa mwenzake Ludovick Rweikiza ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hiyo na kurejeshwa maabusu.

Rwakatare na mstakiwa mwenzake, Rweikiza wanashtakiwa kwa makosa kadhaa yakiwemo ya kupanga njama za kumteka Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msaky, kwa nia ya kumdhuru hali kadhalika kupanga mikakati ya kutenda vitendo vya kigaidi.

Taarifa ya awali chini kabla ya kuachiliwa

Dhamana ya Wilfred Rwakatare Wazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam, imefungua dhamana ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Rwakatare pamoja na mstakiwa mwenzake, Ludovick Josepha Rweikiza.

Miongoni mwa masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama ni pamoja na washtakiwa wote kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya sh milioni 10 kila mmoja na washtakiwa wenyewe kujidhamini. Masharti mengine ya dhamana hiyo ni pamoja na washtakiwa kukabidhi mahakamani hati za kusafiria na kutosafiri nje ya Dar es Salaam bila taarifa.

Kwa uamuzi huo wa mahakama uliotolewa mapema leo, sasa dhamana ipo wazi na kinachosubiriwa ni washtakiwa kutimiza masharti ya dhamana kabla ya kuachiliwa. Rwakatare na mstakiwa mwenzake, Rweikiza wanashtakiwa kwa makosa kadhaa yakiwemo ya kupanga njama za kumteka Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msaky, kwa nia ya kumdhuru hali kadhalika kupanga mikakati ya kutenda vitendo vya kigaidi.