Makocha Sita wa Ireland Watua Kuipiga Msasa Kitayosce FC

UJUMBE kutoka Chuo cha Makocha nchini Ireland umewasili jana, katika klabu ya Kitayosce ya Mjini Moshi kwa ajili ya kushirikiana na kupeana uzoefu.

Ujumbe huo ni wa makocha  6 umewasili na kuanza kazi ya kuinoa timu ya Kitayosce katika uwanja wa King George Memorial, uliopo Soweto Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Klabu ya Kitayosce, Johnson Jabir
mjini Moshi, Kilimanjaro; imeeleza kuwa makocha hao watakaa na timu hiyo kwa muda wa siku 14 kwa ajili ya kuifundisha hasa ikizingatiwa inajianda na michuano mitatu.

Uongozi wa Kitayosce umeitaja michuano hiyo kuwa ni Mkombozi Cup, Marealle Cup na Ligi ya Mkoa. Makocha waliowasili klabuni hapo Conall Walsh, Adam Crowther, Andrew Grehan, John Harrington, Darragh MacGill na Keith McNamara.

Kocha wa Klabu ya Kitayosce Hamad Haule amesema ujio wao utamsaidia kuongeza nguvu katika vikosi vyake katika michauano ijayo. Hamad ameongeza kusema ujio huo ni wa mara ya pili, itakumbukwa kwamba walikuja mwaka jana kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na Klabu yake ilifaidi ujio wao.

Leo ujumbe huo wa makocha umeingia siku ya pili ya mazoezi na Kitayosce FC kwa mazoezi ambapo wachezaji 30 wapo chini yao kwa kuwaongeza vitu adimu katika mchezo wa soka.