Eleuteri Mangi – Maelezo
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limeandaa mafunzo kwa madaktari wa michezo, kinga, tiba na mafunzo ya wataalamu kwa wanamichezo ambayo yatafanyika katika Ukumbi wa Uwanja wa Taifa kuanzia Jumatatu Juni 10 hadi 14, mwaka huu. Hayo yamesemwa na Ofisa Michezo Mwandamizi Baraza la Michezo Taifa, John Chalukulu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
“Lengo kuu la la mafunzo haya ni kuboresha ujuzi wa madaktari na wataalam wa kinga na tiba kwa wanamichezo, sambamba na hilo kuhuisha ufahamu na ujuzi ili kufanikisha uponyaji ulio sahihi na wa haraka kwa wanamichezo waweze kudumu kwa muda mrefu kwenye sekta ya michezo,” alisema Chalukulu.
Bwana Chalukulu alisema kuwa mafunzo hayo yanategemewa kuwa na washiriki wapatao 35 ikiwa ni makadirio ya juu na si chini ya washiriki 15. Aliongeza kuwa mpaka sasa malengo hayo yamefikiwa kwani ni washiriki 16 tayari wamethibitisha kushiki mafunzo hayo.
Kwa upande wake Dk. Anthoni Ngome kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ametoa wito kwa vyama, taasisi na hata watu binafsi kushiriki katika fursa hii adimu ya kuwajengea uwezo madaktari wa michezo nchini.
“Fursa hii imekuja muda mwafaka kwani kuna uhaba mkubwa wa madaktari wa michezo. Nashauri vilabu, vyama, halmashauri na shule mbalimbali walete washiriki katika mafunzo hayo.” alisema Dk. Ngome.
Naye katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Wanamichezo Tanzania (TASMA) Dk. Nassoro Matuzya ameishukuru Serikali kupitia BMT kwa hatua kubwa na ya pekee ya kuanzisha mafunzo hayo kwa kuwa miaka ya nyuma ilikuwa inakosekana.
Mafunzo hayo yataendeshwa kwa pamoja na Wataalamu kutoka wizara husika chini ya Idara ya Michezo kupitia kitengo cha Kinga na Tiba kwa Wanamichezo, Chama cha Wataalamu wa Tiba na Michezo Tanzania (TASMA) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).