Na Mwandishi Wetu, Mbeya
VIONGOZI wenye dhamana ya kusimamia mapato ya ndani katika halmashauri nchini wametakiwa kuboresha miundombinu ya kazi za wakaguzi wa ndani ili kuboresha utawala bora, badala ya kuendelea kufikiria na kujenga dhana kuwa wakaguzi hao wapo kwa ajili ya kuwachimba na kuwaharibia mambo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Msaidizi Bw. Chotto Sendo kwenye kikao cha kazi kilichowahusisha Wakaguzi wa ndani, Mameya, wenyeviti wa kamati za ukaguzi wa ndani na wenyeviti wa halmashauri za wilaya wapatao 90 kutoka mikoa ya Rukwa, Iringa, Mbeya na Ruvuma,kwenye ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya.
Mkaguzi huyo alisema hali hiyo imefanya baadhi ya Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri mbalimbali nchini, kufanya kazi ambazo haziendani na taaluma yao, kutokana na wakurugenzi kutoelewa majumu wanayostahili kufanya watumishi hao. Bw. Sendo alisema kuwa umefikia wakati baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakiwapangia wakaguzi wa ndani kazi za kwenda kukusanya mapato ya halmashauri.
Kutokana na hali hiyo Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali imeanzisha mkakati wa kuimarisha mfumo wa uwajibikaji na Utawala Bora kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) kwa ajili ya kutoa elimu kwa viongozi wa Halmashauri ili watambue majukumu halisi ya wakaguzi wa ndani.
Aidha aliongeza kuwa mpango huo wa kutoa mafunzo utafanyika nchi nzima na umegawanywa katika kanda nne ili kufikisha elimu kwa viongozi wa Halmashauri na wakaguzi wandani ili kuhakikisha kuwa wakaguzi hao wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kupambana na changamoto mbalimbali katika utendaji wao.
Baadhi ya changamoto hizo, Bw. Sendo alisema kuwa ni Baadhi ya Changamoto hizo ni idadi ndogo ya wakaguzi wa ndani ukilinganisha na mahitaji halisi; baadhi ya Sheria na Kanuni kukinzana na Sheria ya Fedha SURA 348 hasa zile za Mamlaka za Serikali za Mitaa, na baadhi ya Maafisa Masuuli kutoshughulikia mapendekezo na ushauri unaotolewa na wakaguzi wa ndani kwa lengo la kuboresha mifumo mbalimbali ya kiutendaji na hivyo kudhoofisha juhudi za Serikali katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali zake, na upungufu wa vitendea kazi na vilivyopo kupitwa na wakati au kuchakaa na hivyo kukwamisha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Nicholous Ntambi alisema kuwa kumekuwepo na madai ya ukandamizwaji wa wakaguzi wa ndani na menejimenti za Halmashauri wa kutotoa rasilimali za kutosha kwa idara ya ukaguzi. Alisema kuwa umefika wakati ambao wakaguzi wa ndani wanastahili kupewa rasilimali na ushirikiano wa kutosha wakati wakitekeleza wajibu wao ili kuleta tija kwenye usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma.
Wakichangia katika mijadala wakati wa mafunzo hiyo washirki waliotoa wito kwa mabaraza ya madiwani kuwa na utaratibu wa kukutana na wakaguzi na kamati za ukaguzi katika halmashauri zao ili kuweza kubaini kama kuna upotevu au utumaiji mbaya wa rasilimali.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Ally Mchucha alisema mbali ya kukutana na wakaguzi na kamati za ukaguzi, aliyataka mabaraza ya madiwani kwa kushirikiana na serikali kuwa pia na utaratibu wa kuafanya tathimini ili kubaini mazingira ya utendaji wa wakaguzi na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali pale zinapotokea.
Naye Mohamed Mwala ambae ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ileje alisema kuwa ushirikiano na wakaguzi kutasaidia kuthibiti tabia ya baadhi ya watendaji wa halmashauri ambao wamekuwa na tabia ya kutokutoa taarifa za za ukaguzi kwa madiwani na pale wakaguzi wa ndani wanapotoa taarifa wanaingiliwa na watendaji wa halmshauri, na kushauri ni vyema idara za ukaguzi wa ndani kuwa nje ya halmashauri.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha Mameya, wenyeviti wa halmashauri kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini pamoja na na wakaguzi wa ndani kutoka kwenye mikoa hiyo ambayo ni Ruvuma, Njombe,Iringa,Katavi,Rukwa na wenyeji wa Mkutano huo Mbeya. Mafunzo hayo yanatarajiwa kugfanyika katika kanda zingine.