Serikali Yaumbuka Sekta ya Elimu

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa

*Kitabu cha hesabu chawapotosha wanafunzi (2X7=15)

SERIKALI imeingia katika kashfa nyingine kwenye sekta ya elimu baada ya kudaiwa kuruhusu vitabu vyenye maelekezo yasiyo sahihi. Mbunge wa kuteuliwa na rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ndiye aliyeanika udhaifu uliomo kwenye vitabu vilivyoidhinishwa na serikali kutumika katika shule za msingi nchini ambapo aliviita ni sumu ya elimu.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Mbatia alionesha vitabu kadhaa bungeni huku akitaja makosa mengi yaliyomo na kuhoji viliidhinishwaje na Kamati ya Kuidhinisha Machapisho ya Kielimu (EMAC).

“Leo tunavuna tulichokipanda. Serikali imetumia fedha za chenji ya rada kusaini mikataba na kampuni zaidi ya 10 kwa ajili ya kusambaza vitabu kwenye shule zetu, lakini vitabu hivyo ni sumu kwa taifa,” alisema.

Alisema kuwa vitabu hivyo vimenunuliwa na fedha hizo sh bilioni 55.2 ambazo zilitengwa na serikali kwa ajili ya manunuzi ya vitabu na mihutasari. Alisema kampuni hizo zilipewa mkataba wa zabuni ya kununua vitabu na mihutasari wa sh milioni 18 na ulisainiwa Machi 18 mwaka huu, huku wakitakiwa kumaliza ununuzi na usambazaji wake Septemba mwaka huu.

Mbatia alisema kuwa vitabu hivyo vikitumika vitalisababisha taifa kufa kielimu kwa vile watoto watajifunza mambo ambayo hayana ukweli. Alitoa mfano wa kitabu cha Jiografia cha darasa la sita kilichoidhinishwa na EMAC ambacho kimekosewa kwa kuandikwa ‘Jografia’.

Vitabu vingine ni cha Hisabati cha darasa la nne katika ukarasa wa 49, ambapo imeandikwa sifuri gawanya kwa sifuri jibu lake ni sifuri wakati jibu sahihi ni haiwezekani. Pia alisema kitabu cha Hisabati kingine kinaonesha 2×7=15 na kitabu cha Uraia pia kinaeleza kuwa ‘mtaa unaundwa na vitongoji mbalimbali na kuongozwa na wenyeviti wa vitongoji.

Mbatia alisema kitabu hicho kinasema kwamba wakazi wengi wa mtaa wameajiriwa na utumishi wa umma, viwanda na makampuni. Alisema kampuni za Macmillan na Oxford zilizopewa jukumu la kuleta vitabu hivyo zimeshafukuzwa nchini Kenya baada ya kugundulika kuwa vitabu vyao havina ubora wa kitaaluma, lakini Tanzania imeendelea kuzikumbatia.

“Kama Rais Kikwete hivi karibuni akiwa Mbeya alikiri kuwa elimu yetu ina udhaifu, kwanini wabunge wa CCM hamtaki kukubali hili?” alihoji Mbatia na kupendekeza iundwe tume ya kudumu ya elimu itakayosimamia maslahi ya walimu, kasoro za elimu na mengineyo.

CCM wapindisha hoja

Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM wamelazimika kupindisha mjadala wa hoja ya udhaifu wa elimu nchini ili kumwokoa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

Hatua hiyo imetokea bungeni mjini hapa ambapo Waziri Kawambwa aliwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2013/14 ambayo ilijadiliwa kwa siku mbili.

Kutokana na upinzani mkali ulioonekana tangu mapema kutoka kwa baadhi ya wabunge hasa wa upinzani, wakitaka Waziri na Naibu wake Philipo Mulugo wajiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012, wabunge wa CCM walilazimika kukutana kwa dharura juzi.

Katika kikao hicho kilichoketi katika Ukumbi wa Pius Msekwa juzi saa 7:00 mchana, wabunge hao wa CCM walifundana na kuafikiana kumwokoa Waziri Kawambwa ili bajeti yake iweze kupitishwa.

Licha ya wabunge wawili wa chama hicho, Deogratius Ntukamazina (Ngara) na Said Mtanda (Mchinga) kuwa wachangiaji wa mapema kabla ya kikao hicho na hivyo kuishambulia wizara hiyo, waliofuata walikuja na visingizio vya kumwonesha waziri hana tatizo.

Katika michango yao, wabunge hao walijiegemeza kwenye hoja ya mgawanyo wa orodha ya shule za sekondari 1,200 zitakazofanyiwa ukarabati wakidai ifumuliwe kwa vile Mkoa wa Kilimanjaro umependelewa zaidi ya mikoa mingine.

Huku wakiunga mkono hoja ya waziri kwa asilimia mia moja na kisha kuanza kulalamikia kasoro zilizopo kwenye elimu, wabunge hao walimtetea Kawambwa kuwa hastahili kujiuzulu kwa vile wizara yake ina majukumu mengi yanayoingilina na Wizara ya Tamisemi.

“Jamani kusema Waziri Kawambwa ajiuzulu tunamwonea, hii wizara majukumu yake mengi yako pia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, atawajibikaje mwenyewe kwa matokeo haya?” walisema.

Katika utetezi huo, waliongeza kuwa bajeti ya wizara hiyo ni ndogo na hivyo waziri amekwama kutekeleza majukumu yake huku wakilibebesha lawama Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) kuwa ndilo limesababisha matokeo hayo kwa kupanga madaraja kimakosa.

Katika hatua iliyoibua msigano, wabunge hao walipendekeza serikali iunde tume nyingine ya wataalamu kuchunguza matatizo ya elimu nchini, jambo lililopingwa vikali na wapinzani wakihoji kwanini walikataa wazo hilo lilipoletwa na Mbatia.

Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, aliwaponda wapinzani akisema kuwa hawatambui kazi kubwa iliyofanywa na CCM na kumtaka Waziri Kawambwa achape kazi bila kuwasikiliza. Aliitaka serikali kutowapeleka walimu wapya vituoni pasipo kuwapa fedha zao za kujikimu kwani inakuwa inatambua idadi yao, lakini akasisitiza kuwa waziri anakwamishwa na watendaji wake.

Peter Serukamba wa Kigoma Mjini, John Komba wa Mbinga Magharibi, Yahaya Kassim Issa wa Chwaka, Jason Rweikiza wa Bukoba Vijijini na Lutengano Kigola wa Mufindi Kaskazini, walilalamikia upendeleo kwenye mgawanyo wa shule, walimu kutopandishwa madaraja na Tamisemi kuondolewa majukumu ya elimu.

Hata hivyo, utetezi huo ulipingwa vikali na wabunge wa upinzani wakidai kuwa katika hilo serikali haiwezi kukwepa lawama kwa Waziri Kawambwa na naibu wake kuwajibika.

“Mimi nilikuwa mmoja wa wabunge waliopinga ugatuaji wa madaraka ya wizara hii kwenda Tamisemi, lakini wabunge wa CCM walitupinga vikali na kupitisha hoja hiyo, sasa leo mnatetea nini?

“Tamisemi iko chini ya Waziri Mkuu, kama leo tunamtetea Kawambwa na kuituhumu Tamisemi ina maana mnataka kusema Waziri Mkuu ndiye hafai,” alisema Mbunge wa Viti Maalumu Susan Lyimo (CHADEMA).

Mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kuwa hakuna tatizo jingine katika Wizara ya Elimu bali viongozi wake hawana uwezo wa kuongoza.

“Tunawaambieni kila siku kuwa hawa watu hawana uwezo wa kuongoza hii wizara…hawawezi, na msipobadilisha hawa watu tutaendelea kuimba nyimbo hizi kila siku,” alisema.

Alisema kuwa serikali inajenga shule mbovu na kuwataka wananchi wapeleke watoto wao huko wakati watoto wa viongozi hawasomi katika shule hizo. Kuhusu Necta, alisema kuwa tangu kuingia kwa Katibu Mtendaji wa sasa, Dk. Joyce Ndalichako na wasaidizi wake, wameziba mianya yote ya wizi wa mitihani.

Mkosamali alisema kuwa wanaompiga vita wakitaka aondolewe ni wale wenye shule binafsi waliokuwa wakisababisha wizi huo ili shule zao zionekane bora.

Joseph Selelasini wa Rombo (CHADEMA) aliwashangaa baadhi ya wabunge kuibebesha lawama Necta kwa kasoro zilizojitokeza kwenye mfumo uliotumika kusahisha mitihani ya dini, ya Bible Knowledge na Islamic Knowledge akisema serikali inaendelea kukiuka katiba kwa kujihusisha na masuala ya dini wakati nchi haina dini.

CHANZO: www.freemedia.co.tz