SINGAPORE itaendelea kuisaidia Tanzania Katika jitihada zake za kuinua elimu na kuongeza ujuzi kwa Watanzania zaidi kupitia mpango wake wa kutoa fursa za mafunzo kwa nchi zinazoendelea. Rais wa Singapore Dr. Tony Tan Keng Yam amemuambia Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Singapore maarufu kama Istana.
“Hatuna Maliasili hivyo tumewekeza zaidi katika elimu na mafunzo kuanzia shuleni, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, tuko tayari kushirikiana na Tanzania katika hili” Dr. Tan amesema.
Singapore inasifika kote duniani kwa juhudi zake chini ya Waziri Mkuu wake wa kwanza Bwana Lee Kuan Yew ambaye aliwekeza na kukazania zaidi elimu ya watu wake kitu ambacho kimesaidia nchi ya Singapore kutoka dunia ya tatu hadi dunia ya kwanza kiuchumi.
Rais Kikwete amewasili Singapore amewasili akitokea Japan ambapo amehudhuria mkutano wa Tokyo unaozungumzia maendeleo ya Afrika -Tokyo International Conference on Africa Development
Rais Kikwete yuko Singapore kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kufuatia mualiko wa Rais wa Singapore.
Akiwa nchini Singapore Rais Kikwete amekutana na wafanyibiashara na kuwakaribisha Tanzania kwa ajili ya uwekezaji ambapo wakuu wa taasisi na sekta mbalimbali wamepata nafasi kuelezea fursa na nafasi za uwekezaji nchini. Mapema leo asubuhi, Rais ameshuhudia utiaji saini wa mikataba kadhaa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore.
Mikataba iliyotiwa saini ni ile ya shirikisho la wafanyabiashara wa Singapore na mfuko wa Sekta binafsi Tanzania(TPSF) , Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Shirika la Intrasia Capital wanaoshughulikia mambo ya nishati, Mamlaka za Bandari Tanzania na Singapore, na kampuni binafsi za Tanzania na Singapore (Pacific International Line ya Singapore na Mac Group ya Tanzania.
Rais Kikwete pia ametembelea bandari ya Singapore, Mojawapo ya bandari tano duniani zinazoongoza kwa utendaji wake bora
Rais pia anatarajia kutembelea Shirika la Nyumba na Maendeleo ya Mji ambalo linasifika kwa kuendeleza miji, ujenzi wa nyumba na makazi ya bei nafuu. Shughuli zingine ambazo Rais anatarajia kufanya ni kutembelea Chuo cha Ufundi cha Singapore na kutembelea maeneo ya viwanda na biashara.
Katika ujumbe wake Rais ameambatana na mawaziri wanao shughulikia maeneo ambayo atatembelea ambayo ni Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe, Waziri wa Viwanda Dr. Abdalah Kigoda, Waziri wa Ardhi na Makazi Prof. Anna Tibaijuka ,Waziri wa Uchukuzi Dr. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Rashid Seif Suleiman.
Wapo pia watendaji wakuu wa mashirika yakiwemo kituo cha uwekezaji nchini cha Tanzania bara na cha Zanzibar (TIC) Na (ZIPA), Shirika la Nyumba (NHC) , Bandari , Shirika la Maendeleo (NDC), Sekta binafsi na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE).
Wengine ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Kituo cha Maeneo huru ya Uwekezaji (EPZA) na Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Chama cha Wafanyibiashara Wanawake Tanzania (TWCC) Chama cha Wanawake wanaojishughulisha na kazi za mikono(TAWOHA), Muungano wa Yyama vya Utalii Tanzania na wafanyibiashara binafsi.
Katika ujumbe wake Rais pia amefuatana na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Mh. Hamis Kigwangala , CCM Nzega , Moses Machali NCCR-Mageuzi, Kasulu Mjini , Mohamed Dewji CCM-Singida mjini, Mh. Silvester Koka , Kibaha Mjini na viongozi wa manispaa za Dar-es-Salaam, Ilala, Temeke, Kinondoni na Mbeya. Rais anatarajia kuondoka Singapore kurejea Dar-Es-Salaam mara tu baada ya kukamilisha shughuli za kikazi tarehe 6 Juni, 2013.