Msafara wa Kamishina Jenerali wa Magereza CGP John C. Minja ukiwasili katika viwanja vya Chuo cha ufundi Ruanda Jijini Mbeya kwa ajili ya kuwatunuku nishani Maaskari wa Jeshi la Magereza.
Kamishina Jenerali wa Magereza CGP John C. Minja akikagua gwaride maalum lililoandaliwa na askari wa Jeshi la Magereza kwa ajili yake mara baada ya kuwasili katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuwatunuku nishani baadhi ya askari wa jeshi hilo.
Baadhi ya maaskari wakisubiri kutunukiwa nishani kutoka kwa Kamishina Jenerali wa Magereza CGP John C. Minja.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jakaya Mrisho Kikwete amewatunuku Nishani mbali mbali Askari 29 kwa Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Nyanda za juu kusini.
Mbali na Nishani hizo pia Jeshi hilo limesema limejipanga kuhakikisha linaanza kujitegemea na kuepukana na Bajeti za Serikali katika kujiendesha kutokana na uwepo wa Rasilimali nyingi zinazoweza kuzisaidia hususani Wafungwa na Ardhi kwa ajili ya kuzalisha Chakula.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamishina Jenerali wa Magereza Nchini, CGP John C. Minja wakati wa hafla fupi ya kuwatunuku Nishani Maaskari wa Jeshi hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Magereza Ruanda Jijini Mbeya.
CGP Minja alisema Jeshi la Magereza linauwezo wa kujiendesha kutokana na kuwa na rasilimali na nguvu kazi ambazo zitatumika katika kuzalisha chakula ili kuepuka kusubili Fedha kutoka Serikalini ambazo huchukua muda mrefu kupatikana na milolongo kuwa mingi.
Aliongeza kuwa hata baada ya kuanza kujitegemea kwa Jeshi hilo kutawapunguzia gharama walipa kodi ambao wamekuwa wakikatwa fedha zao kila siku ili kufanikisha upatikanaji wa Chakula kwa Wafungwa na Shughuli nzima za Jeshi la Magereza Nchini ikiwemo upungufu wa Majengo.
Kamishina huyo pia aliiomba Serikali kuunga mkono juhudi hizo na mikakati ya kutaka kujitegemea ili kuzipunguzia Taasisi Mbali mbali kama Wabunge ambao kila mara wamekuwa wakijadili suala la uboreshaji wa Jeshi la Magereza Nchini.
“ Tangu niingie madarakani lengo langu na ajenda kuu ni kuboresha jeshi la Magereza ili liweze kujitegemea ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia gharama zisizokuwa za ulazima kwa wanaokatwa fedha katika vipato vyao” alisema CGP Minja.
Katika Hafla hiyo Jumla ya Askari 29 walitunukiwa Nishani Kutoka kwa Kamishina Jenerali wa Magereza ambaye alitumia Mamlaka aliyokasimiwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Kifungu cha 34(4) Cha katiba ya Jamhuri ya Muungano ya kuwavisha Nishani Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza ambao walitunukiwa Nishani mbali mbali lakini hawakuvishwa na Raisi Aprili 26, Mwaka huu.
SACP Keenja ambaye ndiye alikuwa akitaja majina ya Askari waliotunukiwa Nishani hizo alisema Orodha ya majina ya Maafisa na Askari pamoja na Nishani zao yameelezwa na kuainishwa katika Taarifa ya Kawaida na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali namba 84/2013 la April 26, Mwaka huu.
Alizitaja Nishani hizo kuwa ni pamoja na Nishani ya Utumishi uliotukuka ambayo hutunukiwa Maafisa waliokwenye Utumishi wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania ambapo kwa Jeshi la Magereza hutunikiwa wenye Cheo cha Mrakibu au wa juu ya Cheo hicho waliotumikia jeshi hilo kwa Miaka 20 Mfululizo ambayo alitunukiwa Askari mmoja ambaye ni ACP Hawa Mollel Simon ambaye pia ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Rukwa.
Nishani ya Pili hutunukiwa kwa Askari kuanzia Nyota Moja ambao wametimiza utumishi wa miaka isiyopungua 15 mfululizo akiwa na tabia njema ya kuweza kusifiwa, Nishani ambayo alitunukiwa Askari mmoja ambaye ni ACP Ally Abdalah Kaherewa ambaye pia ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Ruvuma.
Nishani ya Tatu ni kwa ajili ya askari wenye Cheo cha Wakaguzi, Wakaguzi wasaidizi, Stesheni Sajini, Sajini na Koplo waliotumikia jeshi la Magereza miaka 15 Mfululizo ambayo huitwa Nishani ya Utumishi Mrefu Tanzani ambayo walitunukiwa Askari 18.
SACP Keenja aliitaja Nishani ya nne waliotunukiwa asakari hao kuwa ni kwa wale wanajeshi waliohai ambao walizaliwa Disemba 9, 1961 au kabla ya hapo na mbao wamefanya kazi katika katika Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa muda wa Miaka 35 au zaidi wakiwa Jeshini wenye sifa na tabia njema ambayo huitwa Nishani ya Mwenge wa Uhuru daraja la Nne waliyotunukiwa askari 9.