Baraza la Biashara EAC Lapata Mwenyekiti Mpya

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Jumuia ya Afrika Mashariki, Andrew Luzze Kaggwa

Na Isaac Mwangi, EANA, Arusha

BARAZA la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limemchagua Vimal Shah,Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya BIDCO ya Kenya kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo. Shah alithibitishwa kushika wadhifa huo katika mkutano mkuu wa mwaka wa EABC ulifanyika mwishoni mwa wiki mjini Arusha.

Nafasi hiyo hushikwa kwa mzunguko miongoni mwa nchi tano wananchama wa Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) zinazojumuisha Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi. Safari hii ni zamu ya Kenya.

Aprili mwaka huu, Shah alichanguliwa Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Sekta Binafsi nchini Kenya (KEPSA) na hivyo kumwongezea nguvu pia kwenye nafasi yake ya sasa kiutendaji. Awali Shah alikuwa mjumbe wa Bodi ya EABC.

Anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Gerald Ssendaula wa Uganda ambaye pia alikuwa waziri wa zamani wa nchi hiyo, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.
Waliochaguliwa pia katika mkutano huo kuwa wenyeviti wasaidizi na majina ya nchi zao kwenye mabano ni pamoja na Olive Kigongo (Uganda), Esther Mkwizu (Tanzania), Agatha Juma (Kenya), Alphonsine Nyigema (Rwanda) na Econie Nijimbere (Burundi).

Kila nchi mwananchama pia iliwasilisha na kupitishwa majina ya watu watatu watakaotumikia kama wakurugenzi katika kipindi cha mwaka mmoja ujao wa mhula wa uongozi wao. Alipokuwa anaishukuru timu iliyomaliza muda wake, Shah alisema lengo lake ni kuongeza idadi ya wanachama wa kulipia wa EABC hadi kufikia angalau 250.

Changamoto iliyobainisha ni kwamba baadhi ya vyama vya sekta binafsi hupenda kuyafikisha masuala yao kwenye vyama vya kitaifa zaidi na kuepa kulipa ada ya uanachama wao EABC.