Bajeti ya EAC Yapungua kwa Dola Milioni 10

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na James Gashumba, EANA

MAKADIRIO ya bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyowasilishwa mwishoni mwa wiki kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 imepunguza matumizi yake kwa dola za Kimarekani zipatazo  milioni 10 kwa kulinganisha na matumizi ya mwaka uliopita.

Makadirio ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha umefikia dola za Kimarekani milioni 130.4 kutoka dola milioni 140 za mwaka wa fedha wa 2012/2013,Shirika la Huru la Habari la Afrika Mashairki (EANA) limeripoti.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC ambaye pia ni Waziri wa Nchi anayeshugulikia Masuala ya EAC Uganda, Shem Bageine,aliwasilisha makadirio ya bajeti hiyo kwa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) linaloketi mjini Kampla, Uganda, juzi huku likitoa misisitizo wa utekelezaji wa itifaki ya Soko la Pamoja. Jumuiya hiyo imetenga dola milioni 2.2 kwa ajili ya usalama wa chakula katika kanda hiyo na uhifadhi wa mazingira, hususani ya ziwa Victoria, kwa mujibu wa Bagaine.

 Kiasi kipatacho dola milioni 30 zitatumika katika shughuli mbalimbali za Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria. Maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele katika matumizi hayo ni pamoja na mpango kabambe wa mabadiliko ya tabia nchi na viwanda vya kuongeza ubora wa bihaa zitokanazo na kilimo. 

Katika makadirio ya bajeti yote, Sekretarieti ya EAC itapewa dola za Kimarekani milioni 69.8,EALA dola milioni 13.1 na Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EACJ)  imetengewa dola milioni 4.3.
 Nalo Baraza la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki litapatiwa dola za Kimarekani milioni 9.7 huku dola milioni 3.2 zimetengwa kwa ajili ya Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria.

 Bageine aliliambia bunge hilo kuwa msisitizo mkubwa utawekwa kwenye utekelezaji wa vipengele vya uhuru wa upatikanaji wa ajira miongoni mwa nchi wanachama pamoja na mtangamano wa masoko ya fedha ili kuruhusu uhamishaji wa mitaji. Jumuiya hiyo pia imepanga kujikita katika kuimarisha itifaki ya Soko la Pamoja na kuhitimisha  majadiliano juu ya kuelekea kwenye Itifaki ya Umoja wa Fedha.