Na Anna Nkinda – Yokohama
WAKE wa marais wa Afrika wamefundishwa jinsi ya kutengeneza bidhaa za mikono aina ya mapambo ya nywele na nguo zinatengenezwa na wanawake wengi nchini Japani ambazo zinawasaidia kupata fedha na kuinua kipato cha familia.
Wake hao wa marais akiwemo Mke wa Rais mama Salma Kikwete wamefundishwa jinsi ya kutengeneza bidhaa hizo leo walipotembelea karakana ya bidhaa za mikono zinazotengenezwa kwa Silki mjini Yokohama nchini Japani. Akiwafundisha jinsi ya kutengeneza bidhaa hizo mama Takeyari alisema kuwa vikundi vya wanawake wengi nchini humo vinatengeneza bidhaa hizo kwa kutumia kitambaa aina ya silki.
“Tunatengeneza bidhaa za maua ya kupamba kwenye nywele na nguo ambazo tunaziuza ndani na nje ya nchi na hivyo kujiongezea kipato cha familia”, alisema Mama Takeyari.
Wake hao wa marais pia walitembelea vikundi vya wanawake wanaojishughulisha na kilimo cha mbogamboga vilivyopo eneo la Tsuzuki-ku na kuona mboga za aina mbalimbali wanazozizalisha.
Wanawake hao ambao walikuwa katika vikundi vinne tofauti walisema kuwa walianzisha vikundi hivyo ili kuhakikisha kuwa katika jamii yao kinanapatikana chakula cha kutosha ambacho ni salama.
Mama Yuko morishige alisema, “Tuliona jamii yetu inaishi bila ya kuwa na ushirikiano wa kutosha, kila mtu anaishi maisha yake akitoka kazini anarudi nyumbani na kuendelea na maisha yake tukaona tuanzishe vikundi vya ujasiliamali na maarifa ya nyumbani ili kuimarisha mahusiano baina yetu.
Kutokana na vikundi hivi tumeongeza uzalishaji wa mboga za majani ambazo tunauza na zingine kuzihifadhi kwa ajili ya chakula pia tumeimarisha mahusiano katika jamii yetu”.
Aliendelea kusema kuwa vikundi hivyo vina ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja na vikundi vya wanawake mbalimbali Barani Afrika ikiwemo nchini Bukinafaso ambako wananunua pamba na kutengeneza vazi la taifa la wanawake wa Kijapani linalojulikana kwa jina la kimono.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari walionyesha jinsi ya kuandika maandishi ya Kijapani na kuimba wimbo wa malaika nakupenda malaika ulioimbwa na mwanamziki wa kitanzania Fadhili William ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo na mahusiano mazuri kati ya bara la Afrika na Japani.
Mama Kikwete yuko nchini Japani kwa ajili ya kuhudhulia kongamano la kimataifa la siku mbili la Tuongee kuhusu Ukimwi: Afrika na Japani tushirikiane kutatua changamoto lililoandaliwa na Wizara ya mambo ya Nje ya Japani kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Japani cha mabadilishano na mradi maalum wa wanafunzi kwa ajili ya Mkutano wa tano wa kimataifa wa Tokyo kwa maendeleo ya Afrika (TICAD).