Rais Kikwete aombwa kuendelea kuongoza ALMA

Malabo, Equatorial Guinea

Viongozi  wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wamemwomba Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuendelea kuongoza umoja wa wakuu hao unaopambana na ugonjwa wa malaria – African Leaders Malaria Alliance (ALMA) wakati wanajiandaa na kuangalia jinsi ya kumpata kiongozi mwingine wa umoja huo.

Rais Kikwete amekubali ombi hilo, lakini kwa masharti kuwa anaendelea kuwa Mwenyekiti wa ALMA kwa miezi sita tu ijayo hadi mwenyekiti mpya atakapokuwa amechaguliwa wakati wa Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU uliopangwa kufanyika Januari, mwakani, 2012, katika makao makuu wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.

 

Rais Kikwete amekuwa mwenyekiti wa ALMA tokea kuanza kwake miaka miwili iliyopita na alitarajiwa kukabidhi nafasi hiyo kwa kiongozi mwingine wa Afrika wakati wa Mkutano wa 17 wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa AU ulioanza leo, Alhamisi, Juni 30, 2011 kwenye mji mkuu wa Equatorial Guinea wa Malabo ulioko katika Kisiwa cha Bioko.

Ombi hilo limetolewa kwa niaba ya viongozi wa Afrika na Rais wa Liberia Mama Ellen Johnson Sirleaf wakati wa mkutano wa kazi wakati wa chakula cha mchanauliofanyika kwenye Mgahawa wa La Gaviota ulioko ndani ya kijiji cha Umoja wa Afrika cha Sipopo ambako uko ukumbi wa Palace of Conferences ambako unafanyika mkutano wa wakuu wa AU.

Ombi hilo lilitolewa na Mama Sirleaf hata baada ya Rais Kikwete kuwa amewashukuru na kuwaaga wakuu wenzake wa AU ambao walimchagua kuwa mwenyekiti mwanzilishi wa umoja huo miaka miwili iliyopita baada ya kuundwa kwa umoja huo.

“Mkutano huu unanifikisha mahali pa kukabidhi uenyekiti kwa kiongozi mwingine ambaye tutamchagua. Namtakia mwenyekiti mpya kila la heri na namhakikishia ushirikiano wangu usiokuwa na kifani,” Rais Kikwete amewaambia viongozi wenzake na kuongeza:

“Wakati nafikia mwisho wa uongozi wangu wa ALMA, ningependa kuwashuruku kwa moyo mkunjufu kwa imani yenu kwangu, ushirikiano wenu na kuniunga mkono kwa moyo mmoja. Imekuwa na heshima kubwa kwangu na kwa kweli nimefurahi kupata nafasi ya kutumikia bara letu kama mwenyekiti mwanzilishi wa ALMA.”

Mara baada ya Rais Kikwete kuwa amemaliza hotuba yake ambako aliorodhesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Bara la Afrika katika miaka miwili iliyopita katika mapambano dhidi ya malaria, Rais Sirleaf  ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Alma, ameingia kati na kuwaambia wenzake:

“Hakuna shaka kuwa tumepata mafanikio makubwa katika ALMA katika miaka miwili iliyopita kwa sababu ya uongozi imara na thabiti wa Rais Kikwete. Tunakuomba Mheshimiwa Mwenyekiti uendelee kuongoza Umoja wetu mpaka tutakapoweza kumpata mwenyekiti mwingine.”

Rais Kikwete amesita kwa kama dakika moja tu na hatimaye amesema: “Nakubali ombi la kuendelea na uenyekiti huu lakini kwa muda wa miezi sita tu ijayo. Nitakuwa mwenyekiti wa muda. Lakini lazima tuweze kumpata mwenyekiti mpya wakati wa mkutano wetu ujao, Januari,  mjini Addis Ababa.”

Viongozi wote waliozungumza kwenye mkutano huo wa kazi wamempongeza na kumsifia Rais Kikwete kwa mafanikio makubwa ambayo yamepatikana wakati wa uongozi wake wa miaka miwili. 

Miongoni mwa viongozi waliozungumza kwenye mkutano huo ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Armando Guebuza wa Mozambique, Rais Ellen Johnson Sirleaf, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha Rose Migiro na Rais wa Visiwa vya Sao Tome na Principe.

Kiongozi wa Sao Tome na Principe ametoa hadithi iliyowatia simanzi wajumbe wa mkutano huo wakati aliposema kwake yeye kupambana na ugonjwa wa malaria ni kazi atayoifanya hadi mwisho wa maisha yake kwa sababu mkewe ni mmoja wa wananchi wa nchi yao waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa malaria.

Kiongozi huyo pia amesema kuwa itakuwa kazi ngumu sana kutokomeza ugonjwa wa malaria katika Afrika ifikapo mwaka 2015 kwa sababu mbali mbali hasa kwa kuwa mapambano ya malaria yanahusisha kila mtu.

“Ni kazi kubwa kweli kweli. Katika nchi yangu kwa mfano kuna aina 3,000 za mbu na hatujuia ni mbu gani ni hatari kwa maana ya kusambaza magonjwa ni ni aina gani ina manufaa kwa tabianchi,” amesema huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,

Safarini,

Malabo, Equatorial Guinea.

01 Julai, 2011