Japan Yatangaza Mabilioni Kusaidia Tanzania

Waziri Mkuu Abe pia ameitaka Tanzania na Japan kukamilisha “haraka
iwezekanavyo” majadiliano ya kufikiwa kwa makubaliano ya kulinda
uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ili kufungua njia za uwekezaji zaidi
katika uchumi wa Tanzania kutoka Japan, moja ya mataifa tajiri zaidi
duniani.

JAPAN imetangaza misaada na mikopo ya mabilioni ya fedha kusaidia
uchumi na maendeleo ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kugharamia
uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa miradi ya barabara, ujenzi wa
miradi ya maji, uanzishwaji wa skimu ndogo ndogo za umwagiliaji na
uboreshaji wa kilimo cha mpunga.

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe ametangaza hatua hizo za kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania wakati alipokutana na
kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete.

Viongozi hao wawili wamekutana ofisini kwa Abe
Alhamisi, Mei 30, 2013, mjini Tokyo kwenye siku ya pili ya ziara ya
wiki moja ya Rais Kikwete katika Japan ambako miongoni mwa mambo
mengine amealikwa kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Kujadili
Maendeleo ya Afrika wa Tokyo International Conference on African
Development (TICAD – V) unaoanza Yokohama, mji wa pili kwa ukubwa
katika Japan, keshokutwa, Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, 2013 na
kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Afrika na washirika wa maendeleo wa
Bara hilo.

Miongoni mwa miradi ambayo Japan imekubali kugharimia ambayo baadhi yake inaendelea kujengwa ama karibu inaanza kutekelezwa ni pamoja na
Mradi wa Maji wa Mkoa wa Tabora, Mradi wa Kuboresha Usafiri katika
Mkoa wa Dar Es Salaam ambao ni pamoja na kupanuliwa kwa Barabara ya
Gerezani na Ujenzi wa Daraja Jipya kwenye barabara hiyo, Mradi wa
Kuendeleza Kilimo cha Mpunga nchini na Mradi wa Awamu ya Pili ya
Kuongeza Uwezo wa Serikali za Mitaa kwa Njia ya Mafunzo.

Miradi mipya ambayo Japan itagharimia ni pamoja na Mradi wa Kuendeleza Miundombinu, Mradi wa kujenga skimu ndogo za umwagiliaji, mradi wa ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na kugarimia ujenzi wa barabara
katika milango ya kimataifa ya Mwara, Dodoma na Iringa na Mpango wa 10
wa Kuunga Jitihada za Kupunguza Umasikini.
Wakati wa mazumgumzo hayo, Waziri Mkuu Abe pia ametangaza kuwa Japan itagharamia ujenzi wa barabara za juu kwa juu (fly-overs) kwenye
makutano ya barabara za TAZARA na Ubungo, ujenzi wa mtambo wa
kuchakata umeme wa Kinyerezi ambako unatekelezwa kwa mpango wa Sekta
ya Umma na Sekta Binafsi (PPF).

Waziri Mkuu Abe pia ameitaka Tanzania na Japan kukamilisha “haraka
iwezekanavyo” majadiliano ya kufikiwa kwa makubaliano ya kulinda
uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ili kufungua njia za uwekezaji zaidi
katika uchumi wa Tanzania kutoka Japan, moja ya mataifa tajiri zaidi
duniani.

Abe ameiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za nchi hiyo kujiunga na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) chini ya
mageuzi makubwa yanayotarajiwa kufanyika kwenye mfumo wa Umoja huo.

Rais Kikwete alijibu ombi hilo la Abe kwa kusema:
“Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaunga mkono moja kwa moja jitihada za Japan
kujiunga na Baraza la Usalama kama mwanachama mwenye kura ya turufu.
Unajua msimamo wetu kuhusu jambo hili siku nyingi.”