TANZANIA imesema shughuli ya operesheni za kulinda amani katika mataifa yenye mvutano wa kivita barani Afrika zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upelekwaji wa wanajeshi na udhibiti wa rasilimali na utoaji wa maamuzi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar e s Salaam, Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Emmanuel Nchimbi amesema tunapoadhimisha siku hii pia tunawakumbuka raia, askari na wapiganaji zaidi ya 3,100 waliopoteza maisha tangu mwaka 1948 wakiwa katika zoezi la kulinda amani.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani nchini Tanzania Bw. Richard Ragan akizungumza kwa niaba ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Bw. Alberic Kacou amepongeza vikosi vya Jeshi la wananchi wa Tanzania na Polisi wa Usalama wa Raia kwa kuandaa tukio hilo la kumbukumbu ya walinda amani wa Umoja wa mataifa wake kwa waume waliopoteza maisha yao.
Amesema katika siku hii ya kimataifa, tuitumie kuwakumbuka walinda amani zaidi ya 3,100 waliopoteza maisha na kuwaunga mkono askari zaidi ya 111,000 waliopo na wanaoendelea kulinda amani katika nchi mbalimbali zilizo na migogoro.