Viongozi wa SADC Wampongeza Rais Kikwete

Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameipongeza Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia hiyo chini


WAKUU wa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameipongeza Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia hiyo chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kazi nzuri ambayo Asasi hiyo imekuwa inaifanya kujaribu kutafuta suluhu ya kisiasa katika Madagascar na kuchangia uongozi wa maandalizi ya uchaguzi mkuu katika nchi hiyo mwanachama wa SADC.
Viongozi hao mbali na pongezi hizo, wameitaka Asasi hiyo kuendelea kutafuta njia za kuleta suluhu ya kisiasa katika Kisiwa hicho kikubwa zaidi cha Afrika pamoja na changamoto ambazo Asasi hiyo imekuwa inapambana nazo katika jukumu lake hilo.
Wakuu hao walitoa pongezi zao katika kikao chao kilichofanyika jioni ya Jumapili, Mei 26, 2013 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Viongozi hao chini ya uenyekiti wa Rais Armando Emilio Guebuza za Mozambique walikuwa mjini Addis Ababa kuhudhuria sherehe za miaka 50 tokea kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika na pia kuhudhuria Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU uliomalizika jioni ya Jumatatu, Mei 27, 2013.
Mbali na Rais Guebuza, viongozi wengine wa SADC waliohudhuria kikao hicho ni Mfalme Mswati wa Swaziland, Rais Robert Mugabe w Zimbabwe, Rais Michael Sata wa Zambia, Rais Hefepunye Pohamba wa Nambia, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na wawakilishi wa viongozi wa Malawi, Seychelles, Angola na Botswana.
Katika pongezi zao, viongozi hao walisema kuwa wameridhishwa na kazi nzuri ambayo imekuwa inafanywa katika kutafuta suluhu ya kisiasa katika Madagascar kama kwenye nchi nyingine ambazo zina changamoto za kisiasa kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo pia ni mwanachama wa SADC na Zimbabwe.
Viongozi hao awali walitaka kumpongeza Rais Kikwete peke yake ambaye alipewa jukumu na viongozi wenzake hasa kushughulikia suala la Madagascar ukiondoa DRC na Zimbabwe, lakini yeye mwenyewe aliingia kati na kuomba yafanyike mabadiliko katika Azimio hilo akisema kuwa kazi ambayo amekuwa akiiongoza ni kazi ya wajumbe wote wa Asasi na wala siyo kazi yake binafsi.
Tokea alipochukua uongozi wa Asasi hiyo mwaka jana, Rais Kikwete ameelekeza nguvu zake katika kutafuta suluhu katika migogoro ya kisiasa ya Madagascar, DRC na Zimbabwe na kwa kiasi kikubwa amepata mafanikio katika migogoro yote mitatu hata kama haijamalizika kabisa.
Katika Zimbabwe, mchakato wa Katiba mpya umekamilika na nchi hiyo sasa inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu chini ya Katiba hiyo mpya, na katika DRC Umoja wa Mataifa umekubali kuundwa kwa brigedi maalum ya kijeshi kulinda usalama na amani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Katika Madagascar, Rais Kikwete na Asasi walikuwa wamefanikiwa kuwashawishi washindani na wapinzani wawili wa kisiasa nchini hiyo, Marc Ravalomanana na Rais wa Utawala wa Mpito, Mheshimiwa Andry Rajoelina kutokusimama kama wagombea katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo Julai mwaka huu.
Hata hivyo, katika mazingira ambayo viongozi wa SADC wamesema ni ya kusikitisha sana, viongozi hao wawili baadaye walibadilisha msimamo wao, Mheshimiwa Rajoelina akiwa amejisajili kuwa mgombea urais wakati Mheshimiwa Ravalomanana amemweka mkewe kuwania nafasi hiyo.