Marekani yawaumbua Sitta, Mwakyembe yawasafisha Rostam, Lowassa

Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz

Na Daniel T. Kamna, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, alifanya ziara hapa Tanzania katika shughuli zake mbalimbali nchini alizindua mitambo ya Dowan’s iliyonunuliwa na Marekani na kupewa jina la Symbion.

Clinton amesifu mitambo hiyo ya Dowan’s ambayo awali ilibezwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, Naibu Waziri wa Ujenzi, Harrison Mwakyembe, viongozi wa vyama vya siasa na wanaharakati. Clinton alipigilia msumari wa mwisho aliposema mitambo ya Dowan’s (Symbion) ni mitambo safi na imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa yenye kujali mazingira.

Wahenga walisema; heri ya mtu mchawi kuliko mtu muongo, binadamu muongo anaweza kuleta madhara makubwa kwenye jamii, mfano, nchi kwa nchi kuingia kwenye vita, wananchi kukosa imani na serikali yao, pia ndoa za watu kuvunjika. Njia ya muongo ni fupi, amekuja Mmarekani amenunua mitambo hiyo ya Dowan’s, Waziri Sitta na wenzake sasa wamekaa kimyaa.

Awali ya yote napenda kumpongeza mwanasiasa Kabwe Zitto, aliposimama kidete bungeni bila kujali ametoka upinzani, lakini kwa kujali utaifa wake, alisema mitambo hiyo ya Dowan’s inunuliwe ili kunusuru nchi kuingia gizani, matokeo yake Zitto alishambuliwa na kupewa jina la ‘Kabwe Zitto Fotokopi.’

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Madini na Nishati, Shelukindo, Sitta, Mwakyembe, Mbunge wa zamani wa Nzega, Seleli, katika kundi lao wapo 12, hawa wanafaa kupigwa viboko hadharani na kufukuzwa kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na mateso waliyowapa Watanzania wenzao kukosa umeme kwa sababu ya visasi vyao vya kisiasa.

Wataalamu wa TANESCO wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wao Idrisa Rashid waliitaka Serikali inunue mitambo hiyo ya Dowan’s ambayo ingekuwa mkombozi na kuepusha nchi kuingia katika dhama ya mgawo wa umeme.

Sasa kiko wapi, fedheha kubwa imewakumba Waziri Sitta na kundi lake pamoja na wanaojiita wanaharakati waliokuwa mstari wa mbele kupinga kuwashwa kwa mitambo ya Dowan’s wamezungumza kwenye makongamano, hata kwenye mitandao ya kompyuta (Internet) wamesambaza maneno ya kukashifu mitambo hiyo ya Dowan’s, Waswahili wamenena aliyepewa na Mola amepewa.

Ninatamka bayana kwamba Waziri Sitta, Mwakyembe ndio hasa waliosababisha TANESCO na Serikali kuingia katika matatizo makubwa, hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICC) katika hukumu yake ambayo TANESCO wanatakiwa kuilipa Dowan’s Sh bilioni 94 imechangiwa kwa asilimia 100 na Waziri Sitta, Mwakyembe na genge lao kutokana na husda mbaya dhidi ya wanasiasa wenzao.

Viumbe hawa ni watu wabaya katika jamii, Waziri Sitta anasema eti Serikali haiwezi kununua vitu chakavu, swali kwako Waziri Sitta,  je, vichwa vya treni (stemengene), ndege, je zinanunuliwa mpya? Mitambo ya Dowan’s imekataliwa kisiasa tu.

Ninamuomba Rais wetu mpendwa Rais Jakaya Kikwete, asiwe na kigugumizi katika kutoa uamuzi, mfano kama hii ya Dowan’s. Mtu mwenye akili timamu baada ya ripoti ya wataalamu wa TANESCO kusema mitambo hiyo ya Dowan’s ni mizuri inaweza kukaa miaka 20 bila kufanyiwa ukarabati, tulishangaa Waziri Sitta na kundi lake kupinga kwa nguvu zao zote eti kununuliwa kwa mitambo ya Dowan’s hata kudiriki kusema bora nchi kuingia gizani kuliko kununuliwa kwa mitambo hiyo.

Tulitegemea Rais kutoa uamuzi wa kununua mitambo hiyo kuliko kuyumbishwa na wanasiasa uchwara ambao hawautakii mema utawala wako Rais Kikwete kupata mafanikio.

Mwisho wanasiasa wetu wasiingilie wataalamu wetu kwenye fani zao, wenye fani ya uhandisi ya ujenzi wa barabara, umeme n.k. chonde chonde wanasiasa wetu waacheni wataalamu wetu wafanye kazi ambazo wamezisomea, kodi za wananchi ndizo zimewasomesha wataalamu wetu ili kutoa huduma zinazostahili kwa Watanzania.

Kazi zenu wanasiasa ni kutetea na kuomba msaada serikalini ili wapiga kura wenu wapate maendeleo majimboni kwenu si kuwaingilia wataalamu wetu katika kazi zao. Waziri Sitta, Mwakyembe na kundi lenu msalaba huu wa Dowan’s ni wenu. Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICC) dhidi ya TANESCO walipe Waziri Sitta na Mwakyembe na kikundi chao ikibidi wafilisiwe mali zao kufidia faini hiyo.

Zilizobaki zilipwe na Serikali na TANESCO, sheria ni msumeno, Watanzania hawatawasamehe Waziri Sitta, Mwakyembe mpaka pale watakapoungama hadharani kwamba walidaganya umma na kuapotosha Watanzania juu ya mitambo ya Dowan’s kuhusu watu walio waamini kwa uongo wao.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kupitia 0715 309 669 / 0773 309 669.