Na Anna Nkinda – Addis Ababa
UMOJA WA WANAWAKE wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) umetakiwa kutotegemea fedha za wafadhili katika kujiendesha bali wabuni miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulipaji wa michango yao ya kila mwaka.
Wito huo umetolewa jana na aliyekuwa Rais wa Umoja huo Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba wakati akifungua mkutano wa 12 uliofanyika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mama Pohamba alisema kuwa hadi sasa umoja huo umefanikiwa kuimarika kimawasiliano ya ndani kwa ndani baina ya wanachama wake na hivyo kuweza kuendesha kampeni ya kuondoa na kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo yanasababisha vifo
“Ninawashukuru wanachama ambao wameanza kampeni ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) katika nchi zao, kwa kutoa elimu kwa jamii hii itasaidia kupatikana kwa kizazi ambacho hakina maambukizi ya Ugojwa huu na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto”, alisema Mama Pohamba.
Akiwakaribisha wake hao wa Marais katika mkutano huo mke wa waziri Mkuu wa nchi hiyo Mama Roman Tesfaye alisema kuwa umoja huo ni mzuri kwani unawaunganisha na kuwa kitu kimoja huku wakitimiza majukumu yao katika jamii kutokana na malengo waliyojiwekea.
Mama Tesfaye alisema kuwa tatizo kubwa linaloukabili umoja huo ni upatikanaji wa rasilimali kwani wanategemea fedha kutoka kwa wafadhili lakini kuna baadhi ya wanachama wanaojitahidi kwa hali na mali kuhakikisha kuwa umoja huo unafanya kazi zake bila ya kutetereka.
Wakati huo huo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliwahimiza wake hao wa marais kuunga mkono kampeni ya Shirika la kimataifa la AMREF ya kuwasomesha wakunga 15000 barani Afrika ili kupata wataalamu wengi zaidi ambao watawahudumia kina mama wajawazito wakati wa kujifungua na hivyo kupunguza vifo vyao na vya watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi.
Kampeni hiyo ambayo ilizinduliwa katika nchi mbalimbali Duniani nchini Tanzania ilizinduliwa na Mama Kikwete mwishoni mwa mwaka jana katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar Salaam.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wakisaini kuonyesha kuwa wanaiunga mkono kampeni hiyo wake hao wa marais walisema kuwa kampeni hiyo ni nzuri kwani kama kutakuwa na wakunga wa kutosha vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi vitapungua barani Afrika.
Katika mkutano huo pia ulifanyika uchaguzi wa kumchagua Rais na Makamu Rais wa Umoja huo ambapo Mke wa Rais wa Chadi Mama Hinda Deby Itno alichaguliwa kuwa Rais na Mke wa Rais wa Rwanda Mama Janeth Kagame alichaguliwa kuwa makamu Rais.
Mkutano huo wa wake wa marais wa Afrika ambao ulihudhuriwa na mke wa Rais Mama Salma Kikwete ulienda sambamba na mkutano wa 21 wa wakuu wa nchi na viongozi wa Serikali wa Afrika unaomalizika leo mjini Addis Ababa.