JK Aongoza Ujumbe wa Tanzania Sherehe za AU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete Mkutano wa Sherehe za miaka 50 ya AU katika makao makuu ya umoja huo jijini Addis Ababa leo Mei 25, 2013
PICHA NA IKULU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho
Kikwete amewasili mjini Addis Ababa, Ethiopia, jioni ya
Mei 24, 2013 kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne ambako
atahudhuria Sherehe za Miaka 50 tokea kuzaliwa kwa Umoja wa Nchi Huru
za Afrika (OAU) na baadaye Umoja wa Afrika (AU) na Mkutano wa 22 wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja huo.
Rais Kikwete ambaye anaambatana na Mama Salma Kikwete, ataongoza
ujumbe mzito wa Tanzania kwenye Sherehe hizo za miaka 50 ambao
utawashirikisha marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na
Benjamin Mkapa. Mama Maria Nyerere pia amealikwa kuhudhuria
sherehe hizo katika kundi la Wageni Maalum wa Kimataifa na Kikanda wa
Bara la Afrika.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, atakuwa miongoni mwa
waanzilishi wa OAU. Mwalimu atatambuliwa na kuenziwa kama Mwafrika
Mashuhuri (Pan Africanist Personality) na kwa mchango wao katika
mapambano ya uhuru wa Afrika na kuanzishwa kwa OAU Juni 25, mwaka
1963. Watanzania wengine katika kundi hilo ni Hayati Mzee Rashid
Kawawa na Marehemu Sebastian Challe, Katibu Mkuu wa Kwanza wa
Sekretarieti ya Kamati ya Ukombozi wa OAU.
Katika ujumbe huo wa Tanzania kwenye sherehe hizo atakuwemo pia
Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo kwa
muda mrefu zaidi wa miaka 12 kuliko Katibu Mkuu mwingine, aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro na
aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU Kusini mwa
Afrika Jenerali Hashim Mbita. Ilikuwa wakati wa uongozi wa Salim Ahmed Salim wakati OAU ilipofanyiwa marekebisho na mabadiliko
makubwa kutoka Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na kuwa Umoja wa
Afrika (AU).
Marais hao wa zamani wa Tanzania ni miongoni mwa marais wote wastaafu wa Afrika walioalikwa kushiriki katika Sherehe hizo wakati Salim amealikwa miongoni mwa Makatibu Wakuu wote wa zamani wa OAU na AU. Wengine ambao wamealikwa kwenye sherehe hizi ni marais wa sasa wa nchi wanachama wa Afrika, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa Umoja wa Mataifa kutoka Afrika akiwamo Mama Migiro.
Aidha, AU imewaalika watu mashuhuri walioliletea Bara la Afrika
heshima na sifa kupitia siasa, michezo, muziki na uongozi wa jumuia za
Umoja huo wakiwamo Watanzania –Gertude Mongella ambaye
alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Dkt. Rosebud
Kurwijila ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Masuala ya Kilimo na Uchumi
wa Kamisheni ya AU, na Jenerali Ulimwengu wa Tanzania ambaye alikuwa
kwa miaka mingi akiiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Vijana wa
Afrika mjini Algiers, Algeria.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara ya Rais Kikwete, Jumamosi, Mei
25, 2013, Rais atashiriki katika Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi za AU
na sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwa Umoja huo na
na atahudhuria Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
AU ambao umepangwa kuendelea kwa siku mbili.