Na Hassan Abbas, Addis Ababa
VIONGOZI wa Afrika wameshauriwa kuweka mikakati madhubuti ya kutatua tatizo la ajira kwa vijana ambalo limetajwa kuwa sawa na bomu linalosubiri kuripuka. Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) nao umeshauriwa kufanyiakazi suala hilo.
Changamoto hiyo imetolewa mjini hapa wakati wa mikutano ya kutafakari miaka 10 ya APRM na 50 ya Umoja wa Afrika (AU). Akichangia mada kuhusu utawala bora Barani Afrika, Wakili Maitre Tully kutoka Taasisi ya Kusikiliza Malalamiko ya Wananchi ya Afrika Kusini, alisema sehemu kubwa ya wakazi wa Afrika ya leo ni vijana.
“Takwimu zinaonesha Afrika ina vijana wengi zaidi kuliko sehemu yoyote duniani. Hata hivyo zaidi ya asilimia 60 ya vijana hao hawana ajira,” alisema, hoja iliyoungwa mkono na washiriki wengi wakiwemo wataalamu mbalimbali kutoka APRM.
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa Jopo la Watu Mashuhuri la APRM, Balozi Fatma Ndagiza alitaka vijana wakumbukwe katika mipango ya maendeleo ikiwemo kupewa taarifa juu ya masuala muhimu yanayohusu nchi zao.
Balozi Fatma ambaye alipata kuwa Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, alisema vijana wakipewa taarifa kupitia mitandao ya kijamii watakuwa wamejengewa uwezo wa kujiamini na kushiriki katika maendeleo ya nchi zao.
Akieleza sababu za vijana wengi wa Afrika kukosa ajira, mtaalamu wa masuala ya elimu Prof. Mbaya Kankwenda, alisema elimu inayotolewa Barani Afrika imeshindwa kuzalisha watu “waliona ujuzi na taaluma” bali “wahitimu.”
“Leo Afrika vijana wanasomeshwa kwa kutumia rejea ya vitabu vya maprofesa wa Ulaya ambavyo hata huko Ulaya hakuna anayevisoma,” alisema.
Alisisitiza kuwa vijana wa Afrika sasa wanapewa elimu itakayowapa ujuzi na taaluma mbalimbali zitakazowasaidia kuwa wabunifu katika elimwengu wa sasa unaohitaji watu wenye ujuzi.
Naye Dr. Jean Butera kutoka Rwanda aliwagusa washiriki wengi aliposema kuwa elimu itolewayo sasa kwa vijana haitekelezi ajenda ya kuwasaidia vijana wa Afrika bali “ajenda isiyojulikana.”
“Elimu isiyofuata misingi ya maadili na mahitaji ya Afrika itaishia tu kuwapatia vyeti vijana wetu na si taaluma muhimu. APRM lazima iingilie katika katika eneo hili kwa kufanya utafiti na kuwashauri viongozi wa Afrika juu ya ni mitaala gani inayoweza kuwasaidia vijana wa Afrika kuliko ya sasa?” alitoa hoja.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakipigania kuwepo kwa mikakati nchini ya kusaidia kutatia tatizo linaloongezeka la vijana wengi kukosa ajira.