WAKATI mtu mwingine akiripotiwa kufa, hali bado ni tete katika Mji wa Mtwara kutokana na mabomu ya machozi na risasi za moto kuendelea kurindima kwenye mitaa kadhaa wakati polisi wakipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, linaloaminika kuwa linatokana na risasi.
“Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba akiwa amepigwa risasi tumboni,” alisema Dk Kodi. Inadaiwa kwamba mjamzito huyo ambaye jina lake halikufahamika, ameuawa akiwa nyumbani kwake. Kifo hicho ni cha pili baada ya Karim Shaibu (22), mkazi wa Chikongola kuuawa juzi.
Aidha, kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mtu mwingine ambaye jinsia yake haikujulikana aliuawa kwa bomu la machozi na mwili wake kutawanyika barabarani.
Kuhusu majeruhi, Dk Kodi alisema wamefikia watu 18… “Majeruhi wa mwisho tuliyempokea ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chuno. Alikuwa amevunjwa miguu yote kwa risasi.”
Waomba hifadhi hospitalini
Umati wa watu wengi wao wakiwa kinamama na watoto umemiminika kwenye Hospitali ya Ligula kukimbia msako wa nyumba kwa nyumba unaofanywa na polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamelalamikia kitendo cha polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali zao.
“Magomeni A hatuna amani, askari wanaingia nyumbani kwetu, wanatupiga na kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepotezana na watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema Paulina Idd.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Hadi sasa huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyofunguliwa, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya huku sauti za milio ya mabomu na bunduki ikitawala, wanajeshi waliovalia sare wametapakaa sehemu mbalimbali za mji wakiwa katika magari na pikipiki.
Wakati huo huo; Serikali imesema kwamba imebaini kuwa baadhi ya wanasiasa na taasisi za kiraia wanahusika katika kuhamasisha vurugu zinazoendelea mjini Mtwara.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana Mjini Dodoma, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alirejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba Serikali itawasaka watu wote wanaohusika na vurugu hizo ndani na nje ya nchi bila kujali umaarufu na madaraka yao.
“Baadhi ya taasisi za kiraia na vyama vya siasa kwa masilahi yao binafsi yasiyo na upeo mpana, vinaweza kudhani kuunga mkono madai ya namna hii ni kuimarisha kukubalika kwao miongoni mwa jamii,” alisema Dk Nchimbi: “Tunawakumbusha msemo wa wahenga usemao ‘tamaa mbele, mauti nyuma’… Tunaapa kuwasaka waasisi wa vurugu ndani na nje ya Mtwara, ndani na nje ya nchi yetu.
Wote waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sheria.”
Alisema Serikali inalaani vikali vurugu hizo akisema wanaozihamasisha “wataipasua nchi, watasababisha vifo vya maelfu ya watu, watajaza taifa vilema na majeruhi na hawatanufaika na matokeo haya mabaya.”
Dk Nchimbi alisisitiza msimamo wa Serikali kwamba maliasili hiyo ni ya Watanzania wote… “Tunalo taifa moja la Tanzania ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote. Tabia inayoanza kujengeka ya kila eneo kutaka linufaike peke yake na mali za eneo hilo, italigawa taifa letu vipandevipande.”
Alisema kiini cha vurugu hizo ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam.
Alisema Mei 15, mwaka huu kikundi cha watu kilisambaza vipeperushi kuwataka wananchi wa huko Mei 17, saa 3:00 asubuhi kuacha shughuli na kusikiliza hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kujua mustakabali wa gesi kusafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Alisema juzi, makundi ya vijana yalisikiliza hotuba hiyo maeneo mbalimbali ya Mtwara kama vile sokoni, Magomeni, Mkanaredi na baadaye kupanga mawe na magogo barabarani huku wakichoma matairi.
“Hali hiyo iliendelea kusambaa maeneo mengine ya mji kama vile Chuno, Chikongola, Mikindani na kutoka nje ya mji hadi Mpapura, umbali wa kilomita 40 kutoka Mtwara mjini,” alisema.
Alisema polisi walikabiliana na vurugu hizo na hadi jana, watu 91 walikuwa wanashikiliwa.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz