Mwinyi Ataka Novemba 30 Iwe Mapumziko Afrika Mashariki

Arusha, May 22, 2013 (EANA) – Rais wa zamani wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amependekeza kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutangaza Novemba 30 kuwa siku ya mapumziko kwa nchi zote za jumuiya hiyo ili kuongeza uelewa wa wananchi wake juu ya masuala ya mtangamano.

Novemba 30, 1993 ilikuwa ndiyo siku ambapo Kamisheni ya Utatu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilizinduliwa na hatimaye kuzaliwa upya kwa jumuiya hiyo iliyokufa mwaka 1977. Hivi sasa tarehe hiyo inaadhimishwa kama Siku ya EAC lakini siyo siku ya mapumziko katika nchi wananchama.

Mwinyi alitoa mapendekezo hayo Jumatano jijini Dar es Salaam alipozindua ripoti ya utafiti wa kwanza wa Afrika Mashariki juu ya ushiriki wa raia katika mchakato wa ushirikiano wa EAC, uliyofanywa na Jukwaa la Dira ya Afrika Mashariki (VEAF) ambayo imebaini kwamba upo ushiki hafifu wa raia katika mwenendo mzima wa mchakato huo.

”Nitakuwa na furaha zaidi kutoa mchango wangu wa kuwashawishi marais waliopo sasa ili kutangaza Novemba 30, 1993, siku ambayo Tume ya Utatu ya Afrika Mashariki ilipozinduliwa mjini Arusha, marehemu Mwalimu Nyerere akiwepo, kuwa Siku ya Afrika Mashariki,” alisema Mwinyi ambaye wakati huo alikuwa Rais wa Tanzania.

Alisema, siku kama hiyo wananchi pamoja na mambo mengine wanaweza kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na maonyesho ya utamaduni na bidhaa za kilimo na viwanda katika majiji yote na mipakani, ambapo alisema, mwisho wa siku vitaongeza uelewa wa wananchi juu ya jumuiya yao ya Afrikia Mashariki.

Sehemu ya ripoti hiyo ilisema ingawa kuanzsihwa upya kwa jumuiya hiyo kulilenga iwe na misingi yake kwa wananchi, matokeo ya utafiti huo umebaini kinyume chake.

‘’Theluthi moja ya watu kama wa Tanzania na Kenya hawajawahi kusikia juu ya mtangamano wa EAC,’’ ilisema sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza ‘’ni kwa kuboresha uelewa wa raia juu ya mwenendno mzima wa ushirikiano kwa kushughulikia hofu za wananchi wa pande zote za nchi husika, ndipo awamu hii ya pili ya kihistoria ya kurejesha upya jumuiya hiyo inaweza kufanikiwa.’’

Wanachama wengine wa EAC ni pamoja na Uganda, Rwanda na Burundi.

Akizungumza katika tukio hilo pia, Katibu Mkuu wa zamani wa EAC, Balozi Juma Mwapachu alitaka mwananchi wa kawaida wahusishwe ipasavyo katika mchakato mzima wa mtangamano wa Afrika Mashariki.

”Wana Afrika mashariki wanahitaji kueleweshwa zaidi,kuhamasishwa zaidi na kuwafanya wawe wamoja,” alisema Mwapachu.

Naye Rolf Paasch, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika moja la Ujerumani la Frieddrich-Ebert-Stifstung (FES) nchini Tanzania lilofadhili uzinduzi na utafiti huo alitoa wito kwa wana Afrika mashariki kufanya kila wanaloweza kuhusisha raia katika mchakato mzima wa mtanagamano.

Uzinduzi huo ulihudhiriwa na watu mbalimbali wakiwemo wanachama wa VEAF kutoka EAC,mashirika yasiyo ya kiserikali, waandishi wa habari na taasisi za vijana.

Source: Mtuwa Salira wa EANA

20130523-120106.jpg