Chissano Akemea ‘Urais wa Maisha’ Afrika

Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano

Na Hassan Abbas

RAIS Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano amewataka viongozi wa sasa wa Bara la Afrika kuwa tayari kutetea na kuenzi misingi ya utawala bora Barani humo ili kuwaletea maendeleo raia wao wakati huu Bara hili likiadhimisha miaka 10 ya APRM na miaka 50 ya AU.

Rais Chissano mbali ya kutoa rai hiyo aliwaasa viongozi wa Afrika pia kuenzi utawala bora kivitendo kwa kuwashuri kuachana na dhana ya ‘Urais wa Maisha’ akiutaja mfumo huo kuwa ni miongoni mwa changamoto ambazo ziliifanya Afrika kuonyeshwa vidole kwa miaka mingi.

Bila kutaja kiongozi yeyote kwa jina, Rais Chissano aliyekuwa akitoa hotuba ya kumbukumbu zake kuhusu miaka 10 ya Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), Jumatatu jijini hapa, alisema tofauti na taswira hiyo hivi sasa Afrika imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na katika ujenzi wa demokrasia.

Akiwa yeye binafsi amepata kuondoka madarakani huku akiwa bado kiongozi anayependwa kwa kiasi cha kushinda tuzo ya utawala bora ya Mo Ibrahimu, Rais Chissano alieleza matumaini yake juu ya kuimarika kwa utawala bora Barani Afrika na kupongeza thamani kubwa inayooneshwa na APRM.

“Hivi sasa Bara la Afrika limepiga hatua kubwa katika kuboresha utawala bora na demokrasia. Kuwepo kwa taasisi kama APRM kumesaidia viongozi wenyewe kuamua kuwa wawazi na kukubali kukosolewa.
“Ile dhana ya Afrika kuwa Bara linalosifika kwa viongozi wasioheshimu ukomo wa madaraka yao na hata mapinduzi ya kijeshi vimepungua, “alisema akisisitiza kuwa APRM imekuwa ni maktaba kwa nchi za Afrika kujifunza kutoka zenyewe kwa zenyewe.

Alisema akiwa Rais wa Msumbiji, mwaka 2003 alikuwa mmoja wa viongozi wa AU walioasisi kuunzishwa kwa APRM kwa kuwa Bara la Afrika lilihitaji vigezo vya kujitazama lenyewe kiutawala bora kuliko kutegemea ripoti za nje zilizokuwa kwa kiasi kikubwa hazielezi uhalisia.

Alisisitiza kuwa malengo ya waasisi wa AU ya kuwa na Afrika moja iliyo salama na yenye maendeleo, kwa kiasi fulani yametimizwa kupitia APRM.

“Leo nafarijika kuona tangu pale Maputo mwaka 2003 kikao cha Wakuu wa Nchi za APRM waliporidhia kuanza kazi kwa APRM na zikiwa ni nchi chache sana zilizojiunga, leo ninapoambiwa kuna nchi 33, viongozi wa Afrika wameonesha dhahiri utayari wao wa kuenzi utawala bora,” alisema.

Mkutano huo wa siku mbili wa kujadili miaka 10 ya APRM utafuatiwa na kikao cha Marais wa Nchi za AU zinazoshiriki katika Mpango huo kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki.