Obama Kuzuru Afrika, Mashambulio Iraq 95 Wauwawa

Rais wa Marekani, Barack Obama

RAIS wa Marekani anatarajiwa kuzuru Bara la Afrika mwezi ujao ambako atazuru mataifa ya Senegal, Afrika kusini na Tanzania. Katika taarifa msemaji wa Ikulu ya Rais Jay Carney amesema Obama anapangiwa kufanya ziara hiyo kati ya tarehe 28 mwezi ujao hadi tarehe 3 mwezi Julai ambako atakutana na viongozi wa serikali, biashara na wa mashirika ya kijamii kwa lengo la kuhimiza amani na ustawi wa bara Afrika.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Rais huyo wa Marekani atasisitiza umuhimu wa uhusiano kati ya Marekani na nchi za Afrika ikiwemo kupanua ukuaji wa kiuchumi, uwekezaji na biashara pamoja na kuboresha asasi za kidemokrasia. Mara ya mwisho kwa Obama kuzuru nchi ya bara Afrika ni mwaka 2009 alipozuru Ghana. Rais Obama hatarajiwi kuzuru Kenya.

Mashambulio Iraq 95 Wauwawa

Kiasi ya watu 95 wameuawa nchini Iraq hapo jana katika wimbi la mashambulio yanayowalenga waislamu wa kishia. Mashambulio kumi ya mabomu yaliripotiwa katika mji mkuu Baghdad na mashambulio mengine mawili katika mji unaokaliwa na washia wa Basra ulioko kilomita 420 kusini mashariki mwa nchi hiyo. Zaidi ya watu 150 pia wamejeruhiwa katika mashambulio hayo ya hapo jana.

Zaidi ya watu 240 wameuawa nchini Iraq katika kipindi cha wiki moja iliyopita katika mashambulio kati ya washia wanaoingoza Iraq na waislamu wa kisunni walio wachache na kuzua hofu ya taifa hilo kutumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vilivyoshuhudiwa mwaka 2006. Mashambulio ya hapo jana pia yalilenga maeneo ya wasunni katika mji wa Samarra ulioko kaskazini mwa Baghdad na katika jimbo la Anbar. Marekani imelaani mashambulio hayo na kutoa wito wa kuwepo utulivu nchini humo.

-DW