Wahasibu, wakaguzi 1,911 wafeli mitihani yao

Nembo ya NBAA

Na Joachim Mushi

JUMLA ya Wahasibu na Wakaguzi 1,911 ikiwa ni asilimia 52 ya wahasibu na wakaguzi waliofanya mtihanai wa ngazi ya ATEC I, ATEC II na mtihani wa awali (Foundation Stage A & B), na mtihani wa kati (Intermediate Stage Modules C & D) na mtihani wa mwisho (Final Stage Module E & F) wamefeli mitihani hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu (NBAA) jana ndani ya viwanja vya Saba Saba jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Pius Maneno imeeleza jumla ya watainiwa 1,911 wamefeli kati ya watahiniwa 3,670 waliofanya mtihani huo.

Maneno amesema 740 ikiwa ni asilimia 20.2 wamefahulu mtihani wao na 1,019 ambao ni sawa na asilimia 27.7 watalazimika kurudia mtihani huo kwa masomo walioshindwa katika mtihani huo.

Aidha amesema matokeo hayo ni kwa mujibu wa kikao cha 152 cha Bodi ya wakurugenzi wa NBAA kilichofanyika Juni 30, 2011, chini ya Mwenyekiti Dk. Mussa Assad ambacho kilifanya kazi ya kuidhinisha matokeo ya watahiniwa.

Akifafanua zaidi, Maneno alibainisha kuwa katika ngazi ya mwisho ‘F’ watahiniwa 183 kati ya 869 waliofanya mtihani huo wamefaulu, wengine 316 watalazimika kurudia mitihani yao huku watahiniwa 370 ikiwa ni sawa na asilimia 42.6 wamefeli katika mtihani huo.

Alisema watahiniwa 302 kati ya 2,138 wamefaulu mtihani wa taaluma ngazi ya Module ‘E’ na wengine 431 wanalazimika kurudia somo moja, huku watahiniwa 1,405 hawakufaulu mitihani yao.

“Jumla ya watahiniwa 185 wamefaulu mtihani wa shahada ya juu ya Uhasibu nchini-CPA (T). Idadi hii inafanya jumla ya watahiniwa waliofaulu mitihani ya CPA kufikia 3,608 tangu mitihani hii ianze – mwaka 1975,” alisema Maneno katika taarifa hiyo.

Hata hiyo alieleza kuwa katika ngazi ya awali ya mitihani ya uandishi na Utunzaji wa Hesabu (ATEC I) watahiniwa 54 kati ya 123 wamefaulu mitihani hiyo, huku 53 wanalazimika kurunia na 16 wakiwa wamefeli. Amesema mitihani mingine inatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba Mosi hadi 4 ya mwaka huu.