NMB yawafadhili wajasiriamali kushiriki Saba Saba

Sehemu ya nje ya Banda la Benki ya NMB ndani ya viwanja vya Sabasaba. Nani ya banda hilo imewafadhili takribani wajasiriamali 45 kushiriki katika maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa. (Picha na mpigapicha wa dev.kisakuzi.com)

Na Joachim Mushi

BENKI ya NMB imewawezesha wajasiriamali wa dogo na wakati kutoka mikoa mbalimbali nchini kushiriki Maonesho ya 35 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Jumla ya wajasiriamali 45 wamelipiwa gharama zote za ushiriki wa maonesho hayo ikiwa ni pamoja na nauli na gharama za kusafirisha bidhaa zao mbazo wamekuja kuzionesha katika maonesho hayo, ikiwa ni moja ya mbinu za kuwainua wajasiriamali zinazofanywa na NMB.

Akizungumza na Jambo Leo jana katika banda la NMB, Meneja Mawasiliano wa benki hiyo, Josephine Kulwa alisema wameamua kuwainua zaidi wajasiriamali ili waweze kukua kibiashara kwa kujitangaza na kujifunza changamoto mbalimbali za biashara zao.

Kulwa alisema kuwa NMB imewalipia gharama zote za ushiriki ikiwa ni pamoja na nauli za kusafiri kutoka mikoa wanayotoka na kugharamia usafiri wa bidhaa zao hadi Dar es Salaam kwa ajili ya ushiriki wa maonesho ya mwaka huu, ikiwa ni mpango wa kuwainua wafanyabiashara hao.

Aidha alisema kabla ya kuwaleta wafanyabiashara hao kwenye maonesho waliwapa mafunzo mbalimbali ya kijasiriamali ambayo yaliwaandaa kujua malengo na umuhimu wa ushiriki wa maonesho hayo ya biashara kimataifa.

Akizungumzia vigezo walivyotumia kuwapata washiriki hao, alisema ni wateja ambao wamekuwa waaminifu katika uchukuaji mikopo na urejeshaji wa wakati na wale wenye mwelekeo mzuri wa biashara wanazoendesha na mikopo kutoka NMB. Aliongeza wengine ambao wamepata fursa hiyo ni wale wanaotoka katika klabu za biashara za NMB zilizoko mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Naye mmoja wa wajasiriamali waliopata fursa hiyo kutoka Asasi ya GLORY LUKELO, Doroth Kamala ameusifu mpango wa Benki ya NMB ya kuwawezesha wajasiriamali kushiriki katika maonesho hayo na kuongeza hii ni hatua nzuri ya kuwainua kibiashara.

Kamala ambaye asasi yao inajishughulisha na utengenezaji bidhaa za nguo, kama batiki na mashuka iliyopo jijini Dar es Salaam, alisema anafurahishwa na hatua ya NMB kuwainua wajasiriamali wadogo na wakati kwa kuwapa mbinu anuai za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kutangaza bidhaa zao.