Mama Pinda: Tuombe Yasitokee Mabomu Mengine

Mama Tunu Pinda akiwa na viongozi wa parokia ya Olasiti wakiwaombea Marehemu walio fariki kutokana na bomu lililo rushwa katika kanisa Katoliki parokia ya Olasiti Mkoani Arusha marehemu hao wamezikwa katika eneo la Kanisa mahali Bomu lilipo tupiwa (Picha na Chris Mfinanga)

Mama Tunu Pinda akiwa anampa pole Bibi Consesa Mbaga (43) ambaye nimiongoni wa majeruhi walio lazwa katika Hospitali ya Maunt Meru kutokana na majeraha ya bomu iliotokea katika Kanisa la Katoliki Parokia ya Olastiti na kusababisha vifo na majeruhi katikati ni Dk. Leo Temba. (Picha na Chris Mfinanga)

MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amesema Watanzania wote kwa pamoja wana kila sababu ya kujinyenyekeza mbele za Mungu na kuendelea kuomba ili pasitokee tena ulipuaji wa mabomu kama lile la Arusha.

Ametoa wito huo Alhamisi, Mei 16, 2013 alipokuwa akiongea na Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Padre Prosper Lyimo wakati alipokwenda kwenye nyumba ya Askofu ili kuwapa pole kwa maafa yaliyowapata waumini wa Parokia teule ya Olasiti jijini Arusha, Mei 5 mwaka huu.

Padre Lyimo alimpokea Mama Pinda kwa niaba ya Askofu Mkuu wa jimbo hilo, Mhashamu Josephat Lebulu ambaye alikuwa safarini kikazi akitoa huduma kwa waumini wengine.

Mama Pinda alisema alilazimika kufika kuwapa pole kwa vile alikuwa amewasili mkoani Arusha kwa shughuli ya kikazi. “Wote tumepokea kwa mshtuko taarifa za ulipuliwaji wa bomu pale Olasiti kwa sababu Watanzania hatujazoea mambo ya mabomu. Tunapaswa wote kwa umoja wetu tumuombe Mungu ili atuepushie mabaa mengine…” alisema.

Padre Lyimo aliahidi kuzifikisha salamu za Mhe. Mama Pinda kwa Mhashamu Askofu Mkuu Lebulu na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali hadi chanzo kamili cha tukio hilo kibainike.

Aliwasihi Watanzania kuendelea kuwa na moyo wa kupendana na kushirikiana kwa sababu wote ni wapitaji. “Sote tuko duniani, sote ni wapitaji. Tupendane na tuombeane,” alisema.

Baadaye Mama Pinda alizuru Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia teule ya Olasiti na kupata maelezo kamili kuhusu tukio hilo. Pia alitoa heshima kwa marehemu watatu waliozikwa kwenye uwanja wa kanisa hilo.

Akitoa maelezo hayo mbele ya Mama Pinda, Paroko wa Kanisa hilo, Padre Peddy Castellino alisema ujenzi wa kanisa hilo ulichukua zaidi ya miaka sita kwa kutumia michango ya waumini wenyewe na wala hawakuwahi kupata msaada wowote kutoka nje.

Alisema wao kama kanisa wataendelea kuomba ili tukio hilo liwe la kwanza na la mwisho. “Tunazidi kuomba ili tukio hili lisijirudie tena hapa nchini, na pia tunaendelea kumuomba Mungu ili waliohusika na uovu huu waweze kukamatwa, tunataka kuona mizizi ya matukio haya iking’olewa kabisa na matukio kama haya yasijirudie tena,” alisema.

Alimshukuru Mhe. Mama Tunu Pinda kwa kuwatembelea na kuwafariji na kuongeza kwamba: “Tutaendelea kutetea amani katika nchi yetu ili tunu yetu ya amani isipotee.”

Wakati huohuo, Mama Pinda leo asubuhi amewatembelea majeruhi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini Arusha na kuelezwa kwamba kwenye hospitali hiyo wamebakia wagonjwa 18 na wengine wawili wako katika hospitali ya Elizabeth wakiendelea na matibabu. Wagonjwa wanane walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu Mei 8, mwaka huu.

Mganga Mkuu wa hospitali ya Mount Meru, Dk. Josiah Mlay alimweleza Mama Pinda kwamba wagonjwa wote hali zao zinaendelea vizuri. Watu 66 waliathirika kutokana na mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu ambapo watatu wamefariki dunia