KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilbroad Slaa, Jumatatu, Mei 13, 2013, alikaririwa na gazeti moja akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni, “ilikuwa ikisaka kura kwenye nyumba za ibada na kumwaga sumu mbaya ya udini ambayo sasa inaitesa Serikali na taifa” kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Aidha, katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Dk. Slaa amlipua JK” kwenye gazeti linalounga mkono CHADEMA la Tanzania Daima, Mheshimiwa Slaa anadai kuwa migogoro ya sasa ya kidini “inajengwa au kutengenezwa na Serikali iliyojikita kusambaza sumu ya udini katika misikiti wakati wa kampeni za Urais mwaka 2010”.
Kwa hakika, hakuna namna nyingine ama namna bora zaidi ya kuielezea kauli hii ya Slaa isipokuwa kwamba kauli hiyo ni riwaya nyingine isiyokuwa na mshiko. Ni uongo mtupu. Yake Slaa ni maneno yasiyokuwa na ukweli wowote. Ni uzushi na santuri ambayo imezoeleka sasa kwa wananchi.
Kauli ya Slaa ni mwendelezo wa mtiririko usiokuwa na mwisho wa ghiriba ambazo kamwe hazitafanikiwa za Slaa kuwahadaa wananchi kuhusu ukweli wa mambo ulivyo katika nchi yetu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni kamwe hawakufanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, ama wa mwaka mwingine wowote, katika nyumba yoyote ya ibada iwe msikitini ama kanisani ama hekaluni ama nyumba nyingine yoyote ya ibada mahali popote katika nchi yetu.
Rais Kikwete hajawahi hata kufikiria kuchanganya dini na siasa. Hana sababu ya kufanya hivyo. Anaelewa fika madhara ya udini kwa mustakabali wa nchi yetu, kwa umoja wa taifa letu na kwa mshikamno wa wananchi wake. Yoyote anayejaribu kumbebesha Rais Kikwete msalaba wa udini ana lake jambo na ni vyema atuambie fika Rais alitumia Msikiti upi, ama Kanisa lipi, mahali gani na kwa nyakati gani kufanya kampeni.
Vinginevyo, kauli ya Slaa itabakia ni kauli tu inayostahili kupuuzwa na wananchi, itabakia ni kauli ya mtu mzima anayetapatapa na kufanya jitihada kubwa kujivunjia mwenye heshima kwa kutunga na kusambaza uongo.
Tunanapenda kumshauri Slaa kuwa kama hana jambo la maana la kuwaambia wananchi ama ameishiwa na hoja ni vyema anyamaze, awaachie wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo, kuliko kuendeleza riwaya zake zisizokuwa na mshiko. Yake ni santuri iliyowachosha wananchi.