Mizengo Pinda Azindua Mradi wa Vitabu vya Kieletroniki

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amezindua mradi maalum wa vitabu vya elektroniki vya masomo mbalimbali wenye thamani ya sh. milioni 100 ambao unalenga kupunguza tatizo la ukosefu wa vitabu mashuleni na kuboresha elimu.

Akizungumza na mamia ya wakazi wa vijiji vya Nganana na Nambala wilayani Arumeru mwishoni mwa wiki kwenye uzinduzi wa mradi wa vitabu vya kieletroniki (Nganana E-Reader Project), Waziri Mkuu alihimiza utunzaji wa vitabu hivyo.

“Nimeambiwa kuwa vifaa hivi vina uwezo wa kubeba vitabu 2,000 kila kimoja, na hivyo kutumika kama ‘maktaba za mkononi za vitabu-elektroniki’. Hapa mmepata vifaa vya vitabu-eletroniki 300 na kila kimoja kimewekewa vitabu 100 ndani yake. Sasa ni wapi hapa nchini unaweza kukuta shule au taasisi ambayo inamwezesha kila mwanafunzi kuwa na vitabu 100 yeye peke yake,” alihoji Waziri Mkuu na kushangiliwa.

Waziri Mkuu alisema mradi huo utawasaidia watoto wa shule za msingi za Nganana na Nambala kuongeza ujuzi na kukuza upeo wao wa kuelewa mambo. “Ninawapongeza waliobuni mradi huu kwa sababu vitabu-elektroniki havizeeki wala kuchanika, tofauti na vitabu vya makaratasi, hebu kiangalie ni wakati gani kitu kama hiki kitachakaa,” alihoji.

Alimshukuru Mkurugenzi wa Taasisi wa World Reader ya Marekani, Bw. David Risher kwa kuendesha harambaee huko kwao iliyochangia kupatikana kwa vitabu-elekroniki 200 vya ziada na kuiwezesha Taasisis ya Nelson Mandela kupata vifaa 300 wakati uwezo wao ulikuwa ni kununua vifaa 100 tu. Pia aliushukuru uongozi wa Taasisi ya Nelson Mandela kuwa kubuni mradi huo.

Waziri Mkuu alikabidhi vyeti maalum vya uzinduzi kwa walimu wakuu wa shule za msingi za Nganana na Nambala, Bw. Samuel Pallangyo na Bw. Joseph Mushi.

Akizungumzia taasisi yake ya World Reader, Bw. Risher alisema alisukumwa kuanzisha utunzaji wa vitabu kwa njia ya elektroniki baada ya kutembelea maktaba moja na kukuta imewekewa kufuli kubwa kwa sababu ilikuwa imejaa vitabu viliyopitwa na wakati.

Alisema tangu utotoni, mama yake alizoea kumuacha maktaba wakati yeye (mama) akifanya shughuli zake na kisha kumpitia warudi nyumbani. “Jambo hili lilinifanya nijenge mazoea ya kupenda kusoma vitabu,” alisema.

“Nasi tumeamua kuwasaidia watoto wa Nganana na Nambala, tukiamini kuwa kupitia vifaa hivi vya vitabu-eletroniki, watapata ari ya kujisomea na kujiongezea maarifa. Vifaa hivi siyo vizito na havimpi shida mtoto ya kutembea na mzigo mkubwa wa vitabu, popote alipo anaweza kujisomea ili mradi awe na kifaa chake,” alisema Bw. Risher.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzindia mradi huo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa alisema Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika jitihada zake za kushughulikia masuala yanayoikabili jamii, imebuni mradi huo unaolenga kutumia TEHAMA kuamsha na kuchochea usomaji vitabu kwa kutumia kifaa kinacholingana kwa jirani na simu za mkononi.

“Tegemeo letu ni kwamba wanafunzi wa shule zetu watavichangamkia vifaa hivi na kuvitumia kama ambavyo wanachangamkia simu za mkononi. Ni tegemeo letu kwamba wadau wa elimu vile vile watavichangamkia vifaa hivi ili kuchangia katika kutatua tatizo la ukosefu wa vitabu nchini, na hivyo kuchangia katika kuboresha elimu nchini,” alisema Prof. Mbarawa.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Prof. Burton Mwanilwa akitoa maelezo ya mradi huo alisema chimbuko lake limetokana na nia ya Chuo cha Nelson Mandela kujaribu kutatua changamoto za elimu zinazoikabili jamii. “Chuo kinategemea wanataaluma na wanafunzi wake watoke shule za msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na hizi za Nambala na Nganana ambazo ziko jirani kabisa na chuo chetu,” alisema.

Alisema walipofanya tathmini ya mahitaji, walibaini kuwa wanahitaji E-readers 100 zitakazogharimu dola za marekani 22,000 (zaidi ya sh. milioni 33) lakini kwa vile Chuo hakikuwa na bajeti ya mradi huo, waliamua kuchangisha fedha kutoka kwa wanajumuiya ya chuo, wazazi, wanafunzi na wadau wa mkoa wa Arusha.

“Baada ya kuiona nia yetu ya kulipia E-Readers 100, taasisi ya World Reader ilishawishika kuchangisha fedha huko Marekani na kutuwezesha kuapata E-Readres 200 zaidi na kufanya idadi ifikie E-Readers 300,” alisema.

Alisema walimu 29 walipatiwa mafunzo ya siku mbili na jinsi ya kutumia vifaa hivyo na tayari walikwishaanza kutoa mafunzo ya awali kwa wanafunzi wao. “Matumizi ya maktaba hizi za mkononi ni endelevu, hivyo tunategemea kuwa walimu pamoja na wanafunzi watazichangamkia na kuzitumia ipasavyo ili kuongeza kiwango elimu shuleni,” alisisitiza.