Malecela: Nchi Imepasuka, Aonya Watanzania Mpasuko wa Kidini

Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela


*Kesi ya Lwakatare Kuendelea Leo

WAZIRI MKUU Mstaafu, John Malecela ameonya Watanzania kuhusu mpasuko wa kidini akibainisha kuwa utaigawa nchi vipande vipande, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ametoa wito maalumu akiwataka waumini wa dini tofauti kuvumiliana.

Malecela na Mwinyi walitoa kauli hizo mjini Dodoma na Kibaha, Pwani jana kwa nyakati tofauti, wote wakiwa na nia ya kusisitiza ulinzi wa amani ya nchi inayoanza kutetereka.

Kauli ya Malecela

Malecela alisema kwa namna ilivyo sasa, Tanzania imekuwa ni tofauti na ile aliyoanza kuiona yeye katika kipindi cha uhuru kwenye miaka ya 1960 wakati huo nchi ikiwa moja na watu wake wakiwa ni wamoja.

“Msipokuwa makini na amani yenu, nchi hii mtaigawa vipande vipande na kamwe amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa mambo ya kusingiziana, badala yake tusaidiane sisi kwa sisi, na sisi na viongozi,” alisema.

Onyo la Malecela limekuja kutokana na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mpasuko wa kidini unaoanza kujitokeza nchini.

Malecela alieleza wasiwasi wake juu ya tofauti za kidini katika ibada maalumu ya kuombea amani iliyofanyika katika Kanisa Anglikana Chiwondo lililoko kijiji cha Hombolo katika Manispaa ya Dodoma.

Anafuata nyayo za viongozi wa kitaifa walioonya masuala ya udini kama Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Marais wastaafu, Mwinyi na Benjamin Mkapa pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Alisema waliovamia na kupiga bomu kanisani Arusha ambapo Balozi wa Vatican nchini, Francisco Montecillo Padilla alinusurika kuuawa, si wajinga na wanaweza kufanya mambo kama hayo eneo lolote nchini.

 “Kujenga nchi ni kazi ngumu sana lakini kuibomoa ni kitendo cha muda mfupi ambacho kinaweza kufanyika kwa kutumia sekunde chache ni lazima kuisaidia serikali katika kuitafuta amani,” aliongeza Malecela.

Malecela ameonya baadhi ya watu kutochukua sheria mikononi kuhusu yale yanayowapata na badala yake waiachie Serikali yao kufanya uamuzi wa nini kifanyike ili amani ibaki.

Lwakatare kupigania dhamana yake Kisutu leo

Wilfred Lwakatare (kulia)


JOPO la mawakili wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare leo linaanza harakati za kumtoa mahabusu kwa dhamana.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana na kubaki na shtaka moja la kula njama ambalo linadhaminika.

Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2013, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatajwa leo, lakini mawakili wa Lwakatare wamejipanga kumwombea dhamana Lwakatare. Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatala aliliambia Mwananchi jana kuwa kwa kuwa kosa lililobaki linadhaminika, basi jambo moja watakalolifanya leo ni kuwasilisha maombi ya dhamana.

“Kwa kuwa shtaka lililobaki linadhaminika na kwa kuwa tayari file (jalada) la kesi limesharejeshwa (Kisutu) kutoka Mahakama Kuu, basi tutakachokifanya kesho (leo) ni kuomba dhamana tu,” alisema Wakili Kibatala na kuongeza:

“Kama hapatakuwa na pingamizi lolote tunaamini kuwa leo anaweza kutoka kwani tumejiandaa kutekeleza masharti yoyote yatakayotolewa na mahakama.”

Ikiwa hapatakuwa na pingamizi lolote la kisheria kutoka upande wa mashtaka ambalo litaibua mabishano makali, huenda mahakama ikatoa uamuzi wa maombi ya dhamana leo, na kama watuhumiwa wataweza kutimiza masharti yatakayowekwa na mahakama, basi Lwakatare anaweza kurejea uraiani leo.

Hata hivyo, kama kutakuwa na pingamizi la kisheria na mabishano mahakama, inaweza kuahirisha na kupanga siku nyingine ya kutoa uamuzi wa maombi hayo ili kupata muda wa kutafakari kwa kina hoja za kisheria za pande zote zitakazokuwa zimetolewa.

Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati ya hayo yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai. Mashtaka hayo yalikuwa ni kula njama, kupanga kumteka Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu na kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi.

Mashtaka hayo matatu yalikuwa yakiwakabili washtakiwa wote wawili wakati shtaka la nne la kuhamasisha vitendo vya ugaidi lilikuwa likimkabili Lwakatare peke yake, akidaiwa kuruhusu nyumba yake ya Kimara King’ongo kutumika kupanga mipango ya ugaidi.

Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka matatu ya ugaidi na kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na maombi ya jopo la mawakili wa Lwakatare waliyoyawasilisha mahakamani hapo wakiiomba ipitie uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwafutia kesi ya awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi ya mashtaka hayohayo.

CHANZO: www.mwananchi.co.tz