Na Said Ameir, Ikulu Zanzibar
SERIKALI ya Falme za Kiarabu (UAE) iko tayari kusaidia kuimarisha hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ili iweze kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi. Balozi mpya wa nchi hiyo Abdulla Ibrahim Al-Suwaidi ametoa kauli hiyo Ikulu leo wakati alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika mazungumzo hayo Balozi Abdulla alisema nchi yake inajivunia uhusiano wake wa kihistoria na Zanzibar na kwamba iko tayari mbali ya sekta ya afya kuisaidia sekta nyingine ikiwemo elimu. Amesema wakati wa kipindi cha kuitumika nchi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha uhusiano huo unaimarika kwa kuangalia maeneo zaidi ya ushirikiano ikiwemo biashara na uwekezaji.
Alimueleza Rais kuwa ujumbe wa wafanyabiashara kati ya 40 na 50 unatarajiwa kuzuru Tanzania mwezi Juni mwaka huu ili kujionea fursa za biashara na uwekezaji na hiyo itakuwa fursa nyingine ya kuimarisha mahusiano kati ya serikali na watu wa Falme za Kiarabu na Tanzania.
Akimkaribisha Balozi huyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza balozi Abdulla kuwa Zanzibar imetiwa moyo na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na nchi za Falme za Kiarabu na kuzishukuru kwa misaada mbalimbali ambayo Zanzibar imekuwa ikipata kutoka nchi hizo.
Alieleza miongoni mwa sekta zilizofaidika ni maji na afya ambapo hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ilifanyiwa ukarabati mkubwa miaka ya nyuma. Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza balozi huyo mipango ya serikali ya kuifanya hospitali hiyo kuwa ya rufaa kwa kuweka vifaa vya kisasa na kuiwezesha kutoa huduma zote muhimu kwa wagonjwa.
Rais alikubaliana na rai iliyotolewa na Balozi Abdulla ya kuongeza ziara za viongozi hasa mawaziri na watendaji wakuu wa serikali za nchi zao ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha uhusiano wa Serikali na watu wa nchi mbili hizo. Alisema ziara hizo ni muhimu katika kujenga msingi imara wa ushirikiano ambao alisema serikali na watu wa nchi mbili hizo wana kila sababu kufanya hivyo kuendeleza maslahi ya pamoja.
Dk. Shein alipendekeza ujumbe wa kibiashara kutoka Falme za Kiarabu utakaotembelea Tanzania mwezi Juni upangiwe ratiba ya kuzuru Zanzibar ili kutoa fursa ya kuiona Zanzibar na kukutana na viongozi wa Serikali na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima wa Zanzibar.
Dk. Shein alielezea pia umuhimu na kuhimiza uanzishwaji wa safari za moja kwa moja za ndege za mashirika ya nchi hizo kama vile shirika la ndege la Emirates na Al –Arabiya ili kuimarisha biashara na utalii Zanzibar.