Na Immaculate Makilika- Dodoma
WANANCHI kusafiri kutoka Mtwara hadi Bukoba kwa barabara ya lami. Hayo yamesemwa bungeni mjini Dodoma wakati Waziri wa Ujenzi John Magufuli alipokuwa akijibu swali la Martha Mlata (Viti Maalum-CCM), lililohoji juu ya ahadi ya Serikali katika kipindi cha Awamu ya Nne na iliyosema wananchi wataweza kusafiri kwa taxi toka Mtwara hadi Bukoba; Je, utekelezaji wa ahadi hiyo umefikia wapi.
Aidha Waziri Magufuli alisema kuwa nia ya msemo huo ni kuonesha kwamba wananchi wataweza kusafiri toka Mtwara hadi Bukoba kwa lami na kuongeza kuwa lengo hilo limetekelezwa kwa mafanikIo makubwa hadi kufikia asilimia 99 ya barabara yote kutokea Mtwara hadi Bukoba.
Hata hivyo Magufuli aliendelea kwa kwa kusema kwamba barabara yote kuanzia Mtwara – Dar es Salaam- Dodoma-Singida- Nzega-Tinde-Usagara pamoja na Geita-Bwanga-Kyamyorwa hadi Bukoba yenye urefu wa kilometa zipatazo 1,989 imejengwa kwa kiwango cha lami.
Isipokuwa sehemu fupi yenye urefu wa takribani kilometa 26 katika barabara ya Ndundu-Somanja ambayo itakamilika kujengwa kwa kiwang o cha lami kabla ya Desemba, 2013. Alisema Serikali ya awamu hiyo itahakikisha ahadi ya wananchi kusafiri kwenye barabara ya lami toka Mtwara hadi Bukoba inatekelezwa.
Wakati huo huo, SERIKALI imesema kwamba wafungwa na mahabusu wanayo haki ya kupata huduma bora za Afya kama ilivyo kwa raia wengine. Ili kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya magerezani, Jeshi la Magereza limeajiri Wataalamu wa Afya wa fani mbalimbali kama vile madaktari, madaktari wasaidizi, wauguzi, maafisa afya, wataalamu wa lishe, wataalamu wa Maabara hali kadhalika na wahudumu wa Afya.
Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alipokuwa akijibu swali la Mariam Nassoro Kisangi (Viti Maalum-CCM) lililohoji Je, Serikali ina utaratibu gani wa kutoa huduma za Afya kwa wafungwa waliopo magerezani.
Naibu Waziri huyo alisema kwamba kila Gereza lina Zahanati ndani na nje ya Gereza. Zahanati za ndani ya Gereza hutumika kutoa huduma za tiba kwa wafungwa na mahabusu na zahanati za nje hutoa huduma kwa watumishi, familia za watumishi na wananchi waishio jirani.
Aidha, inapotokea tatizo la mgojwa linahitaji uchunguzi au huduma nyingine ambazo hazipo katika kituo husika, mgonjwa hupewa rufaa kwenda kutibiwa katika hospitali ya Mkoa au Wilaya iliyokaribu. Kwa wale wenye matatizo yanayohitaji huduma za madaktari Bingwa, Wafungwa na Mahabusu hupewa rufaa kwenda kutibiwa katika hospitali za rufaa au hospitali maalumu kama vile Muhimbili, KCMC, Bugando, Mbeya, Ocean Road na Mirembe alisema Naibu Waziri huyo.
Hata hivyo changamoto zilizopo ni uhaba wa madawa ambao haukidhi mahitaji kutokana na ufinyu wa bajeti na vilevile ukosefu wa magari ya kuwapeleka wagojwa hospitali. Aidha Jeshi la Magereza linafanya jitihada za kuwajumuisha wafungwa na mahabusu katika mfumo wa matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya.