Wafugaji Waongezea Pato la Taifa

Nchi yetu inajitosheleza kwa mahitaji ya nyama  ambayo kwa mwaka tunazalisha wastani wa tani 462,686, kwa mchanganuo wa nyama ya ng’ombe tani 248,108, nyama ya mbuzi/kondoo tani 92,351, nyama ya nguruwe tani 39,676 na nyama ya kuku tani 82,551.

Na Immaculate Makilika- Dodoma

SERIKALI  yawapongeza wafugaji  wote nchini kwa mchango wao  mkubwa unaoliwezesha  Taifa kutoagiza nyama toka nje  ya nchi  na badala yake  kuliingizia kipato kutokana  na mauzo ya mifugo  hai na nyama nchi za nje.
Hayo yamesemwa  Bungeni leo na Naibu Waziri  wa Maendeleo  ya Mifugo na Uvuvi , Benedict  Ole Nangaro ,wakati wa kipindi cha maswali na majibu, hata hivyo  Naibu Waziri   huyo alisema kwamba  mwaka 2011/2012, ng’ombe 3,362 na mbuzi/kondoo 4,060 wenye thamani ya Sh. Bilioni 3.81 waliuzwa nje.

Aidha tani 31.6 za nyama ya ng’ombe ,tani  647 za nyama  ya mbuzi na tani 151.8 za nyama ya kondoo ziliuzwa nje na kulingizia Taifa  takribani Sh. bilioni  19.3
Fedha iliyookolewa kwa kutoagiza nyama kutoka nje haiwekwi kama akiba mahsusi   bali hutumika kwa maendeleo  ya sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo.

Nchi yetu inajitosheleza kwa mahitaji ya nyama  ambayo kwa mwaka tunazalisha wastani wa tani 462,686, kwa mchanganuo wa nyama ya ng’ombe tani 248,108, nyama ya mbuzi/kondoo tani 92,351, nyama ya nguruwe tani 39,676 na nyama ya kuku tani 82,551.

Hata hivyo, kutokana na mahitaji ya soko hususani wageni toka nje ,baadhi ya hoteli za kitalii na migodi  huagiza tani 800 za nyama maalumu kwa mwaka ,kiasi kinachogharimu Sh. bilioni 10.2.
Serikali inaendelea kuwahimiza  wafugaji kufuga  kibiashara  na kuzalisha nyama  bora ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani  na nje ikiwemo migodi.