MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa tayari hatua kubwa imeshafikiwa kwa upande wa Zanzibar katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM zikiwemo kusimamia utekelezaji wa sera ya hifadhi na maendeleo ya wanawake na haki zao.
Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi Tawi la CCM Majenzi, Micheweni Pemba akiwa katika uendelezaji wa ziara zake za chama zilizoanza kisiwani Pemba baada ya kumaliza Unguja.
Katika maelezo yake, akiwahutubia mamia ya wana-CCM waliohudhuria sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi, Dk. Shein alisema kuwa Ilani ya Chama chake imemtaka kuwaangalia wanawake.
Alisema kuwa Serikali iliyoko madarakani imo katika kutekeleza Ilani ya CCM kwani ndio chama kilichoshinda uchaguzi ambapo katika utekelezaji wake wanawake nao wameweza kupewa kipaumbe katika masuala mbali mbali ikiwemo elimu, afya, ajira na mengineyo.
Alieeleza kuwa tayari serikali imeshatenga skuli maalum kwa ajili ya wanawake ikiwemo skuli ya Bembella kwa Unguja na Utaani kwa Pemba pamoja na kuwaendeleza katika vyuo vikuu kwa asilimia kubwa.
Kwa upande wa sekta ya afya, Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuhakikisha akina mama wanapata huduma za afya zilizo bora ikiwa ni pamoja na kutolipia huduma za kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Kutokana na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa hatua hiyo, Dk. Shein aliziagiza Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Afya kutafuta ameagiza Wizara ya Afya kumtafuta wakala wa uhakika atakayeleta dawa na vifaa kwa ajili ya huduma hiyo kwa wakati, hatua ambayo itatekelezwa katika Bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2013/14.
Akieleza juu ya suala la ajira, Dk. Shein aliwasihi vijana kutochagua kazi na kusisitiza kuwa serikali inaendelea na juhudi za kuwajengea mazingira bora vijana ya kujiajiri wenyewe kutokana na ajira za serikali kutotosheleza mahitaji ya walio wengi.
Alisema kuwa tayari ameanza kuchukua jitihada za utekelezaji wa kuanzisha Mfuko maalum wa kuwasaidia vijana na akina mama, chini ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji wananchi Kiuchumi na Ushirika mfuko ambao umechangiwa na wahisani kadhaa na si muda mrefu atauzindua.
Katika maelezo yake, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar aliwapongeza wanachama wapya 60 waliojiunga na CCM kutoka chama cha CUF Tawi la Maziwang’ombe Jimbo la Micheweni.
Akieleza kuhusu Muungano, Dk. Shein aliwataka wana-CCM na wananchi wa Micheweni kuutunza na kuuenzi Muungano kwani umeleta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili za Muungano hasa Zanzibar.
Alieleza kuwa tayari changamoto za Muungano zimeshafanyiwa kazi na kusisitiza kuwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano una changamoto zake na sio Zanzibar pekeendiy yenye changamoto za Muungano.
Sambamba na hayo, Makamu alisisitiza kuwa siasa ni ustaarabu wa maisha na wala sio chuki, uhasama na kutishana.
Akimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, aliutaka uongozi wa Mkoa kuhakikisha wale wote waliojiunga na CCM hawapati vitisho wala bughudha kutokana na uamuzi wao wa kukihama chama cha CUF kwani hiyo ndiyo demokrasia.
Mapema Makamu alipokea taarifa ya wana-CCM wa Wilaya ya Micheweni katika ukumbi wa Jamhuri, Wete Pemba, ambapo katika taarifa yao walieeleza kuwa hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa ndani ya Mkoa huo ni tofauti na ile iliyokuwa mara tu baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi.
Dk. Shein alianza ziara yake kwa kuweka jiwe la msingi Tawi la CCM Kifundi linaloendelea kujengwa. Kiasi ya Tsh. Milioni 12.5 zilikuwa zinahitajika kumalizia ujenzi huo na ndipo alipopitisha harambee kwa wana-CCM na viongozi waliohudhuria katika hafla hiyo ambapo zaidi ya Tsh. Milioni 8.2 zilichangwa. Dk. Shein mwenyewe alichangia Tsh. Milioni 3.
Baada ya hapo aliwasili Maskani ya CCM ya Shamsi Vuai na kukagua miradi ya wanamaskani wanaotengeneza vitambaa vya batiki wa UWT na kuweka jiwe la msingi Tawi la CCM Majenzi na baadae kuwakabidhi kadi wanachama wapya 224 wakiwemo 60 kutoka CUF.
Katika Tawi hilo pia, viongozi na wanachama wa CCM walipitisha harambee kwa ajili ya kumalizia tawi hilo ambapo zaidi ya Tsh. 8.7 zilipatikana.