Na Immaculate Makilika- Maelezo
SERIKALI imeandaa mkakati wa kuendeleza kilimo cha kahawa ( Tanzania Coffee Industry Development Strategy,2012-2022) kwa lengo la kuendeleza kilimo cha zao hilo nchini kupitia Bodi ya kahawa nchini na kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.
Aidha Serikali imefafanua kuwa hatua hiyo ni kuongeza uzalishaji ,tija na ubora wa kahawa Kitaifa ili kuboresha mapato ya wakulima wa zao hilo katika mikoa mbalimbali inayolilima ikiwemo mkoa wa Kilimanjaro .
Kauli hiyo ilitolewa leo Bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Mahusiano na Uratibu Steven Wassira kwa niaba Waziri wa Kilimo ,Chakula na Ushirika , Chrisopher Chiza , wakati akijibu swali la Grace Kiwelu(Mbunge Viti Maalum-CHADEMA) aliyeuliza Je,Serikali ina mpango gani madhubuti na mahsusi wa kufufua kilimo cha Kahawa mkoani Kilimanjaro ambacho kwa miaka mingi kimekua tegemeo kwa wananchi wa Kilimanjaro na mhimili mkubwa kwa uchumi wetu wa Taifa letu.
Alisema malengo mahsusi ya mkakati huo ni pamoj ana kuongeza na uzalishaji wa kahawa safi kutoka wastani wa sasa wa tani 50,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 100,000 ifikapo mwaka 2022 na kuongeza ubora wake ili kupata bei ya ziada katika masoko ya nje kutoka wastani wa asilimia 35 hadi kufikia wastani wa asilimia 70 ifikapo mwaka 2022.
Aidha Wassira alisema maeneo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugavi ili wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo,kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora ya kahawa ,pamoja na kuongeza matumizi ya viwanda vya kati vya kuitayarisha ili kuongeza ubora wa zao hilo na hivyo wakulima kunufaika na bei nzuri.