Awamu ya Pili ya NEEC kuiwezesha mikoa 5

Ofisa Mwandamizi, Uhusiano wa Umma na Ushawishi wa NEEC, Edward Kessy

Na Joachim Mushi

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi (NEEC), limeongeza mikoa mingine mitano zaidi ambayo wananchi wa mikoa hiyo wataanza kunufaika na fursa ya uwezeshaji kupitia shughuli za kilimo hasa cha umwagiliaji pamoja na ufugaji kimakundi.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mwandamizi, Uhusiano wa Umma na Ushawishi, Edward Kessy alipokuwa akifanya mahojiano na mtandao huu ndani ya viwanja vya Maonesho ya 35 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika Dar es Salaam.

Ofisa huyo alisema mikoa ambayo itanufaika katika bajeti ya NEEC awamu ya pili ni pamoja na mikoa ya Shinyanga, Dodoma, Pwani, Tanga na Mkoa wa Ruvuma, ambapo wananchi katika vikundi watawezeshwa kupata mikopo hasa kwa miradi ya kilimo cha umwagiliaji ili kuwainua kimaisha.

Kessy alisema utaratibu ambao utafanywa na NEEC ni kama uliofanyika kwa awamu ya kwanza, ambapo baraza hilo litaweka dhamana kwa Benki ya CRDB na vikundi hivyo vya wananchi kupatiwa mikopo zaidi ya mara tatu ya dhamana iliyowekwa na NEEC.

Alisema kuondezeka kwa mikoa hiyo kunatimiza idadi ya mikoa 10 ambayo hadi sasa baadhi ya vikundi kutoka mikoa hiyo vimenufaika na kuitaja mikoa iliyonufaika katika awamu ya kwanza kuwa ni pamoja na Lindi, Mtwara, Manyara, Singida na Mkoa wa Rukwa.

Alibainisha kuwa katika awamu ya kwanza zaidi ya watu 4,000 wamenufaika kutokana na fursa inayotolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, hivyo kuwataka wananchi kushiriki kwa kufuata masharti ya kuingizwa katika fursa hiyo.

Akizungumzia vigezo vya mikoa inayoteuliwa kuingizwa katika uwezeshaji huo na masharti, Kessy alisema mikoa inayopewa kipaumbele ni ile ambayo ipo katika hali ya chini katika upatikanaji huduma za kifedha kuwainua wananchi.

“Kwa kweli tumefanikiwa kwa kiasi fulani maana watu walionufaika na fursa zetu hali zao ya maisha zimebadilika tofauti na awali…tunayo mifano katika Mkoa wa Mtwara, kilimo cha korosho na Manyara kilimo cha mpunga, hii pia ni kwa maeneo mengine tuliyoyafikia,” alisema Kessy.