Rais Kikwete Awapongeza Wanabahari Kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani

Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza wanahabari, wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari nchini kwa kuadhimisha Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani (World Press Freedom Day) Mei 3, akiwahakikishia kuwa Serikali yake itaendelea kukuza, kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari ulioshamiri kwa kiwango cha juu kabisa nchini kwa sasa.

Aidha, Rais Kikwete amesisitiza kuwa Serikali yake na yeye binafsi, kama mdau wa habari, wataendeleza kuelekeza nguvu kubwa katika kupanua Uhuru wa Habari kwa sababu uhuru huo ni kigezo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania na katika kujenga na kupanua demokrasia nchini.
Katika salamu zake kwa wanahabari, wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari nchini ambayo inasherehekea Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Dunia kitaifa mjini Arusha leo katika shughuli zilizoandaliwa na Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Tawi la Tanzania, Rais Kikwete amesema:
“Kama muumini na mdau wa Uhuru wa Habari ambao ni sehemu ya Uhuru Mpana Zaidi wa Kutoa Maoni (Freedom of Expression), napenda kuwapongezeni wanahabari wote nchini na wadau wenzenu duniani katika kusherehekea siku hii ya kuadhimisha Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ambayo kitaifa hapa kwetu inaadhimishwa na shughuli zilizoandaliwa na MISA-Tan mjini Arusha.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais: “Sisi katika Tanzania tunayo kila sababu ya kusheherekea Siku hii ya leo ya Uhuru wa Habari nchini kwa sababu sote ni wadau wa habari ni mashahidi wa mafanikio makubwa na mengi katika nyanja ya habari katika miaka 20 iliyopita katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, naungana nanyi katika kusheherekea na kuadhimisha mafanikio haya makubwa.”

Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ambayo chimbuko lake ni Mkutano wa Waandishi wa Habari wa Afrika waliokutana na kutoa Tamko la Windhoek (Namibia) – the Windhoek Declaration on Promoting an Independent and Pluralistic African Press pamoja na kuanzisha Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika – Media institute of Southern Africa (MISA), Mei 3, mwaka 1991, ilichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya Uhuru Duniani mwaka 1993.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Napenda kutumia Siku hii ya leo kuwapongezeni tena kwa kazi yenu nzuri ambayo imeendelea kuchangia maendeleo ya nchi yetu kupitia njia ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha wananchi. Vile vile, napenda kutumia nafasi ya Siku ya leo kuwaelezeeni utayari wa Serikali yetu kuendelea kuithamini kazi hii nzuri. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuifanya kazi yenu kwa kuongozwa na misingi mikuu ya weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha, kama ambavyo tumekuwa tukifanya, napenda kuwahakikishieni kuwa mimi binafsi na Serikali ninayoingoza nitaendelea kushirikiana nanyi katika kupanua, kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari nchini ikiwa ni haki ya waandishi kufanya kazi yao kwa mazingira mwafaka ya kisiasa, kiuchumi, kisheria na kijamii. Vile vile, napenda kuwahakikisheni tutaendelea kushirikiana nanyi katika kulinda uhuru wa wapata habari nchini ambao ni muhimu kama ulivyo uhuru wa vyombo vya habari.”