KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema ina ushahidi unaoonyesha njama za kuhakikisha kuwa ni wana CCM pekee, ndiyo watakaochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara. Imedai kuwa njama hizo zimepangwa na ngazi za juu za chama hicho.
Akitoa maoni upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema Machi 3, mwaka huu siku mbili baada ya Mwongozo wa Tume kuanza kutumika, Katibu wa NEC ya CCM (Uhusiano wa Kimataifa), Dk Asha-Rose Migiro alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC-CCM inayoonyesha kujipanga kuingia kwenye mabaraza peke yao.
“Barua pepe ya Dk Asha-Rose Migiro inasema “Sambamba na hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya Mwongozo wa Tume, sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea,” Lissu alinukuu barua pepe hiyo.
Lissu alisema baada ya Dk Migiro kuagiza alimalizia kwa maneno yafuatayo: “Tafadhali wanakiliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.”
Aliwataja waliopelekewa nakala ya barua pepe ya Dk Asha-Rose Migiro, kuwa ni Mwigulu Nchemba, Zakhia Meghji, Muhammed Seif Khatib na Nape Nnauye.
Lissu alisema siku moja baadaye, Nape aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake akiwashauri ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa suala hilo, wapate taarifa kila siku kuhusu hali halisi inavyoendelea katika kila mkoa na kwamba ni vizuri idara ikaandaa orodha ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda vizuri au la!
Alisema njama za CCM kuteka nyara mchakato pia zinahusu uhalalishaji wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni na kwamba, Desemba 18, mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Francis Mwonga, aliwaandikia barua makatibu wote wa CCM wa mikoa na kuwapa maelekezo ya kikao cha Sekretarieti.
“Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi,” alisema Lissu akimkariri Mwonga.
Lissu alisema maneno hayo yaliandikwa hata kabla Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, tayari Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani, kufanya mawasiliano na ‘wahusika’ kuhusu jinsi ya kupanga vituo vya kupigia kura.
Alisema mawasiliano hayo ya viongozi wa ngazi za juu za CCM, yanathibitisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya umeingiliwa na kuhujumiwa kwa kiwango kikubwa na CCM.
Pia, alisema mawasiliano hayo yanathibitisha kauli iliyotolewa bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wakati wa mjadala wa hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba viongozi wa Serikali walihamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kuwa wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa Chadema wanaenguliwa chaguzi za vijiji, mitaa au kata.
CHANZO: Gazeti Mwananchi