Mei Mosi Yaadhimishwa kwa Ghadhabu

Waandamanaji nchini Uhispania wameandamana kupinga ukosefu wa ajira

SIKU KUU ya wafanyakazi ulimwenguni imesherehekewa leo kwa maandamano na ghasia katika nchi mbali mbali. Nchini Ugiriki wanafanya mgomo kupinga sera za kukaza mkwiji na Bangladesh wakipinga mazingira hatari ya kazi.

Shughuli nyingi zimepooza nchini Ugiriki kufuatia mgomo wa saa 24 uliotangazwa na vyama vikuu viwili vya wafanyakazi, ambao wanalalamikia sera chungu za kubana matumizi zinazotekelezwa na serikali yao, ikitimiza masharti ya wakopeshaji wa kimataifa. Safari za gari moshi na feri zimeahirishwa na watumishi wa hospitalini hawakuripoti kazini leo.

Police wapatao 1000 wanashika doria katika mji mkuu, Athens tayari kuingilia kati ikiwa ghasia zitaibuka katika maandamano hayo. Hata hivyo, idadi ya wanaandamanaji inatarajiwa kuwa ndogo ikilinganishwa na mwaka jana ambako wafanyakazi 100,000 waliandamana.

Wafanyakazi Bangladesh wameandamana kupinga vifo vya wenzao walioangukiwa na kiwanda Mwisho wa uvumilivu

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya umma Ilias Iliopoulos amesema, ”Ujumbe wetu unaeleweka vizuri, tumechoka na sera hizi ambazo zinaumiza watu, na kuwafanya masikini kuwa masikini zaidi.” Iliopoulos ameongeza kuwa serikali yao inapaswa kuachana na sera hizo, kwa sababu wananchi wamefika kwenye kikomo chao cha uvumilivu.

Nchini Uturuki nako, polisi wametumia magari kuwamwagia maji waandamanaji waliojikusanya mjini Istanbul na katika miji mingine ya nchi hiyo, hali ambayo imegeuka utamaduni nchini humo kila ifikapo tarehe mosi mwezi Mei. Waandamanaji hao walikuwa wakijaribu kuvivunja vizuizi vya polisi.

Na huko Bangaladesh, wafanyakazi ambao wameghadhabishwa na vifo vya wafanyakazi zaidi ya 400 walioangukiwa na kiwanda wiki iliyopita, wameingia mitaani wakitaka wamiliki wa kiwanda hicho watiwe kitanzi. Mmoja wa viongozi wa wafanyakazi katika viwanda vya nguo nchini humo Kamrul Anam, amesema kuwa wafanyakazi wanasikitishwa na kile alichokiita mauaji dhidi ya wenzao.

”Tunataka waliosababisha msiba ule wapewe adhabu kubwa kuliko zote” amesema Anam.

Polisi wa Bangladesh wanakisia kuwa idadi ya walioshiriki katika maandamano mjini Dhaka inafikia watu 10,000 huku idadi hiyo ikitegemewa kuongezeka.

Waandamanaji nchini Uhispania wameandamana kupinga ukosefu wa ajira Tukirudi barani Ulaya, mandamano yamefanyika katika miji 80 ya Uhispania, ambako idadi ya wasio na ajira imepanda na kufikia asilimia 27. Katika mji mkuu wa Italia, Roma, vyama vya wafanyakazi vimeandaa tamasha la muziki, kushinikiza mabadiliko katika sera za kubana matumizi ambazo zinakumbatiwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Maandamano mengine kuhusiana na siku kuu ya wafanyakazi ulimwenguni yameripotiwa nchini Indonesia kupinga hali duni ya wafanyakazi wa nchi hiyo, na huko Ufilipino ambako wafanyakazi wanadai nyongeza ya mshahara na mazingira bora ya kazi.

Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis amewatolea mwito viongozi wa kisiasa kufanya kila juhudi kuongeza nafasi za kazi, akisema ukosefu wa ajira umesababishwa na mtindo wa kiuchumi, ambao unapuuza mipaka ya haki za kijamii.

-DW